HAFLA YA KUMKABIDHI MKANDARASI MRADI WA UJENZI WA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI KIZAGA-NDAGO -SEPUKA YENYE UREFU WA KM 77.6
BASHUNGWA AMKABIDHI MKANDARASI HENAN BARABARA KM 77.6 SINGIDA
Waziri wa Ujenzi Mhe. innocentbash ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kumsimamia kikamilifu Mkandarasi Henan Highway Engineering Group anaejenga barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga KM 77.6 ili ikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Amesema hayo Misigiri Iramba mkoani Singida katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway ujenzi wa barabara hiyo.
" TANROADS jipangeni vizuri ujenzi ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora", amesema Mhe. Bashungwa.
Waziri huyo wa ujenzi amewataka wananchi watakaopata ajira katika mradi huo kuwa waaminifu, wabunifu na walinzi wa vifaa vya mkandarasi ili kutouchelewesha mradi huo na kujiongezea ujuzi ili utakapokamilika wawe wamenufaika maradufu.
" Tunataka mradi huu uendane na thamani ya fedha na barabara hii kwakuwa itachochea uchumi ni vema wananchi mkatumia fursa za biashara na uzalishaji wa mazao zitakazosababishwa na uwepo wa barabara hii kukuza uchumi", amesema Waziri Bashungwa.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema barabara hiyo inayounganisha wilaya za Singida, Ikungi na Iramba itahuisha uchumi kwa wakazi wa mkoa wa Singida kwa kuwa inapita kwenye maeneo ya kilimo na madini.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni 88.5 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo.
Nae Mbunge wa Iramba ambaye pia ni Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba ameishukuru Serikali kwa namna inavyozifungua barabara za mkoa wa Singida na kuwataka wakazi wa mkoa huo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan Mkoa huu umepewa Sh.bilioni 210 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara. Bw, Peter Serukamba amhakikishia Waziri wa Ujenzi kuwa vifaa vya mkandarasi vitalindwa na atapata ushirikiano ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
“Tunaishukuru serikali kwa kuwa barabara zetu kubwa mkoani singida zinajengwa kwa kiwango cha lami na hivyo kuufanya mkoa wetu kufikika kirahisi toka pande zote za nchi nasi tumejipanga kuongeza uzalishaji wa vitunguu, alizeti,ufuta,mahindi na ufugaji wa kuku”, amebainisha mkuu wa mkoa Serukamba
Amesema hayo (Septemba 10, 2023) wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi wa kampuni ya Henan High Way Engeneering Group mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka -Ndago hadi Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 ambayo Serikali imetoa Sh.bilioni 88 kwa ajili kuijenga kwa kiwango cha lami.
Serukamba amesema pia katika kipindi hicho Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) Mkoa wa Singida umepatiwa Sh.bilioni 34 ambapo miradi kadhaa imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82 lililojengwa kwa Sh.bilioni 32, daraja a Msingi mita 100 kwa Sh.bilioni 11.9 na ujenzi wa barabara ya Itigi yenye urefu wa kilometa 10 kwa Sh.bilioni 8.9.
Aliongeza kuwa barabara ya Itigi kwenda Mbeya zimetengwa Sh.bilioni 60 na kwamba barabara zote zinazoendelea kujengwa mkoani hapa zikikamilika Singida itakuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao mbalimbali ambayo yatafikishwa kwa urahisi kwenye masoko yaliyopo ndani na nje ya mkoa.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Serukamba amesema Mkoa wa Singida umepanga katika msimu wa kilimo mwaka huu kulima ekari milioni moja za alizeti kutoka ekari 681,000 zilizolimwa msimu uliopita lengo ni kuhakikisha mafuta ya kula ya kulisha nchi nzima yawe yanatoka Singida.
"Kuna miradi 12 ya mabonde ya umwagiliaji kwa Mkoa wa Singida ambayo ujenzi wake upo katika hatua mbalimbali, tukimaliza miradi ya umwagiliaji yote vitunguu vyote vya nchi hii ufuta, dengu, pamba, korosho, mahindi, mafuta ya alizeti vitatoke Singida,"alisema Serukamba..
Kuhusu mbolea, Serukamba amesema maelekezo ya Wizara ya Kilimo yalishatolewa ambapo ifikapo Septemba 20, mwaka huu mbolea itakuwa imefika kila Wilaya.
"Mwaka huu niwahakikishie wana Singida hakuna kijiji ambacho mbolea haitafika, kazi imeanza na maafisa kilimo safari hii sitawaachia tutasimamia mimi na ma-DC (Wakuu wa Wilaya) wangu kuhakikisha mbolea na mbegu inafika kwa wakati ili watu wasipate sababu, nataka safari hii tuongeze uzalishaji wa mazao," alisema.
Serukamba akizungumzia maji, alisema katika vijiji 441 vilivyopo katika mkoa huu asilimja 66 vinapata huduma ya maji na mjini upatikanaji wa maji ni asilimia 85 na malengo ifikapo 2025 upatikanaji wa maji vijijini itafikia asilimia 80 na mjini asilimia 100.
Kuhusu umeme amesema vijiji 341 kati ya 441 vilivyopo mkoani hapa vimepata umeme na vijiji 100 vilivyobaki wakandarasi wapo kazi wakiendelea na kazi na ni matumaini ifikapo mwakani vijiji vyote vitakuwa vimefikiwa na umeme.
"Sisi wanaSingida tuna deni kwa Rais Samia Suluhu Hassan na tuna shauku kubwa sana kumlipa deni na deni hili tutaanza kulilipa 2024 na kumalizia 2025, wanaSingida wanamwelewa sana Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Serukamba.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa innocentbash akimkabidhi Cheti cha Pongezi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Bwana Michael A. Matomora kwa kusimamia Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba na Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 hadi 2025
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), (kulia) akipokea cheti cha kutambua mchango wake katika maendeleo ya mkoa wa Singida kutoka kwa Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb), wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi, Kampuni ya Henan Highway Engineering Group Ltd, mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kutoka eneo la Sabasaba-Sepuka-Ndago hadi Kizaga, yenye urefu wa kilometa 77.6, utakaogharimu shilingi bilioni 88.6, hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Misigiri, Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, jana.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.