HATIMAYE Halmashauri za Wilaya ya Iramba Mkoani Singida na Meatu Mkoani Simiyu zimekubaliana kwa pamoja kufunga Ziwa Kitangiri ili kuboresha mazingira ya mazalia ya samaki kwa manufaa ya Halmashauri hizo.
Makubaliano hayo yamefanyika juzi katika kikao cha pamoja cha Ujirani mwema kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Meatu Mkoani Simiyu ambapo Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya hizo wakiongozwa na Wakuu wa Wilaya hizo ambao ni Wenyeviti wa kamati za Ulinzi na usalama.
kikao hicho kiliwakilishwa na Simon Tyosela Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iramba, Pius Machungwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, kamati za Ulinzi na Usalma za Wilaya zote, Madiwani, pamoja na wakuu wa Idara.
Akifungua kikao hicho cha Ujirani mwema Mkuu wa Wilaya ya Meatu Dk. Joseph Chilongani alisema kuwa, imekuwa jambo zuri kwa kamati za Ulinzi na Usalama pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri zote mbili na baadhi ya Madiwani wa Halmashauri kuwa na kikao cha pamoja cha kuhakikisha tunalinda Ziwa Kitangiri kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Halmashauri hizo.
‘’ Ni jukumu letu sisi viongozi wa Wilaya hizi kuhakikisha tunatunza na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Kitangiri ili kutoa fursa samaki wazaliane kwa wingi na wakubwa kwa ajili ya kitoweo kwa jamii na kuwaongezea kipato wananchi kwa ujumla pamoja na kuongeza mapato ya Halmashauri zetu.’’
‘’ Cha msingi Halmashauri wilaya za Iramba Meatu, Igunga na Wilaya ya Kishapu tulikuwa na utaratibu wa pamoja za Kufunga Ziwa Kitangiri kila mwaka lakini hatukuwa mpango mkakati wa pamoja kuamua ni lini ziwa hili litakuwa linafungwa kila mwaka, hata hivyo katika kikao cha Ujirani mwema tuliofanya mjini Shinyanga mwaka juzi tulikubaliana kuhifadhi Ziwa Kitangiri na kupiga vita kwa nguvu uvuvi haramu na kuhakikisha mazingira ya Ziwa yanakua mazuri ili samaki wazaliane kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.’’ Alisisitiza Dkt. Chilongani
Alipokuwa Katika Kijiji cha Usulize Wilayani Meatu kwenye kambi ya wavuvi ya kijiji hicho alitangaza rasmi kufunga Ziwa hilo.
‘’ Mkuu wa Wilaya ya Iramba na Wenyeviti wa Halmshauri zote na kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya hizi leo hii natamka kuwa Ziwa Kitangiri limefungwa hadi tarehe 01 mwezi Aprili mwaka huu hivyo kuanzia tarehe 17/04/2019 ndiyo Ziwa litafunguliwa Rasmi na shughuli za uvuvi zitaanza tena na yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria’’ alionya Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula alisema tayari kwa upande wa Wilaya ya Iramba Ziwa Kitangiri limeshafungwa toka tarehe 01 mwezi Januari na litafunguliwa tarehe 01 mwezi Aprili 2019
‘’ Ndugu Mkuu wa Wilaya ya Meatu kwa upande wetu tulikwisha funga Ziwa Kitangiri kama kawaida yetu ya kila mwaka isipokuwa mwaka huu tumeona tuje kujiriridhisha katika Wilaya ya Meatu maana miaka yote sisi tulikuwa tukifunga Ziwa upande wa Meatu wanavua hii ilikuwa inawatia unyonge sana wavuvi wa upande wa Iramba’’
‘’ Kwa hiyo hivi sasa tutahakikisha kwamba zuio la uvuvi liheshimiwe na ifikapo tarehe iliyopangwa mvuvi yeyote atakayeonekana katika kambi za uvuvi au Ziwani akivua samaki itakuwa halali yetu, hatutakubali watu wanaharibu mazalia ya samaki tukiwaangalia tu . hata Ziwa likifunguliwa ni marufuku kutumia nyavu zinazotumika katika uvuvi haramu, itafanyika dori ya nguvu kuhakikisha Ziwa hili linalindwa kwa nguvu zote’’ alisistiza Mhe: Luhahula
Kikao hicho cha ujirani mwema kimewaeleza wataalamu wa Halmashauri za Wilaya za Meatu, Iramba, Kishapu na Igunga ambao wananchi wake wanaonufaika na Ziwa hilo watengeneze Rasimu na kuweka sheria ndogo ndogo za kulinda Ziwa hilo na wamepewa mwezi mmoja kuandaa rasimu hiyo ambayo itakuwa ndiyo dira ya kudhibiti Ziwa hilo lisihujumiwe.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.