Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kutunga Sheria ndogo itakayotumika kuzuia mifugo wanao randaranda mitaani na kufanya uharibifu wa miti iliyopandwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya.
Maelezo hayo ameyatoa leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo alipokuwa akitatua kero za Wananchi waliokuwa wakilalamikia uwepo wa mbuzi wanaozurura mitaani na kuharibu miti na mazao mengine yaliyopandwa.
Akitolea ufafanuzi swala hilo Mkuu wa Mkoa huyo amemuagiza aliyekuwa akikaimu nafafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri Husseni Sepoko kuhakikisha kwamba katika kipindi kifupi wawe wametunga Sheria ndogo ambazo zitawasaidia kuzuia wanyama wanaorandaranda ambayo itaruhusu kukamata mifugo hiyo na kuwapiga faini.
"Nakuagiza Mkurugenzi katika kipindi kifupi kijacho mtunge Sheria ndogo ambazo zitazuia mifugo kuzurura mitaani, na mhakikishe Sheria hiyo inaweza kutoa adhabu kali kwa watakao kiuka utaratibu". RC Serukamba
Amesema kwa sasa ni mpango wa Mkoa kuhakikisha kwamba kunapandwa miti zaidi ya Milioni tatu na kuifanya Mkoa Singida kuwa wa kijani jambo ambalo haliwezi kufanikiwa endapo miti hiyo itaendelea kuharibiwa na mbuzi wazururao.
"Mkoa tumepanga kupanda miti zaidi ya Milioni tatu, tutashirikiana na wanafunzi, Makanisa na Misikiti kuhakikisha kila kaya inakuwa na miti isiyopungua minne, hatutavumilia jitihada hizo zikwamishwe kwa uzembe" Serukamba.
Aidha amewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanawafuata wananchi walipo na kutatua kero zao badala ya kukaa ofsini kusubiri viongozi wa ngazi ya juu wanapotoka na kila mtumishi ahakikishe anakamilisha majukumu yake kwa wakati.
Akiwa katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ameweza kusikiliza jumla ya kero 32 zikiwemo za ardhi, maji na madeni na usafi wa Mazingira.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.