Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Emmanuel Luhahula amewataka wawekezaji wazawa waliopo kwenye taasisi mbalimbali na wadau wengine wanaowekeza kufuata taratibu za Nchi za uwekezaji.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito huo juzi wakati akipokea msaada wa vitanda 21 toka Shirika la Sadeline Health Care lenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika nje ya jengo la Halmashauri hiyo mjini hapa.
“Mkurugenzi wa Sadeline, Sara Kitainda nakushukuru sana kwa msaada huu, nina uhakika kuwa vitanda hivi vitawasaadia akina mama sehemu ya kulala ili wajifungue vizuri katika Hospitali yetu” ameshukuru na kuongeza kuwa
“Lazima turudishe shukrani kwenu maana kitendo hichi kinatufariji sana, na tunatoa wito kwa wasomi wote walioko kwenye taasisi mbalimbali kuendelea kuiunga mkono Wilaya yetu kwa kujitolea misaada mbalimbali”
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanavitunza vizuri vitanda hivyo ili viweze kuihudumia jamii kwa muda mrefu.
“Niombe Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha mnavitunza vizuri vitanda hivi ili vifanye kazi iliyokusudiwa kwa sababu leo hii sisi tupo kesho hatupo na tunatamani wanaokuja waendelee kufaidika na matunda ya vitanda hivi,” amesisitiza Luhahula
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sadeline Health Care, Sara Kitainda amesema kuwa vitanda hivi vimetoka katika Shirika la Rotary Club toka nchini Canada ambavyo vimegharimu takribani tsh 32.3milioni.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, leo hii nimefarijika sana kukukabidhi vitanda 21 kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma za Afya katika Hospitali yetu ya Kiomboi ili akina mama waweze kujifungua wakiwa mahali salama,” amesema Kitainda
Hata hivyo Kitainda ameongeza kuwa lengo la taasisi yao ni kusogeza huduma katika Wilaya hii hivi karibuni kwa kuanzisha tawi la taasisi hiyo.
“Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana nasi katika jitihada za kutoa huduma mbalimbali katika wilaya yetu. Taasisi yetu inatarajia kufanya kampeni ya kuhamasisha wananchi kupima tezi dume kwa njia ya kisasa pamoja na kupima shinikizo la damu bure.”
Halikadhalika, Sara ametoa wito kwa wataalam mbalimbali wa afya ikiwemo waliokwisha staafu hususan walioko nje ya Nchi na ndani ya Nchi ambao ni wazaliwa wa Wilaya hii kutoa ushirikiano wa dhati kusaidia Wilaya hii kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt Adam Mashenene ameishukuru taasisi hiyo ya Sadeline Haelth Care na kuahidi kutoa ushirikano pindi taasisi hiyo itakapoka fungua tawi lake Wilayani Iramba.
Hata hivyo Dkt Mashenene ameahidi kuvitunza vitanda hivyo kwa manufaa ya jamii kwa ujumla ili viweze kutoa huduma kwa muda mrefu.
Taasisi ya Sadeline Health Care yenye makao yake Makuu jijini Dar es Salaam imekuwa na utaratibu wa kuchangia vifaa vya huduma za Afya ambapo mwaka juzi ilitoa vitanda 18 na hivi karibuni Taasisi hiyo inatarajia kutoa mashuka Wilayani hapa.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akikagua vitanda vilivyo tolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sadeline Health Care, Sara Kitainda. Picha na Hemedi Munga
Vitanda mbalimbali vya kisasa vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sadeline Health Care, Sara Kitainda ili kusaidia huduma za Afya Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.