MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Mama Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kukagua na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya cha Kinampanda, Ukarabati wa chuo cha Ualimu Kinampanda, Kiwanda cha kukamua Mafuta ya alizeti cha YAZA tarafa ya Ndago na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Akizungumza na wananchi wa Iramba, makamu wa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe: Mama Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Iramba katika kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. “Nawapongeza sana wananchi wa Iramba kwa Mapokezi makubwa, mmejitokeza kwa wingi na mmekuwa mstari wa mbele kushirikiana katika shughuli za maendeleo kwa nguvu zenu zote. Dumisheni ushirikiano, Amani na utulivu ndani ya maeneo yenu Alisema Mhe: mama Samia.
Makamu wa Rais, alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa mkoa wa Singida kwa kile alichodai kwamba toka ameanza ziara yake hadi anamaliza, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ambayo ina thamani inayofanana na fedha zilizotumika.
Aidha makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Mama Samia Suluhu Hassani ameagiza leseni 40 zilizo futwa na Wizara ya Madini Mkoa wa Singida wapewe wazawa wachimbe ili waweze kunufaika na kuleta Maendeleo katika Mkoa wa Singida.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo baada ya Waziri wa Madini, Mhe: Dotto Biseko, kusema wamefuta leseni hizo baada ya wahusika kushindwa au kuchelewa kuanza kuchimba madini hayo kwa wakati.
Mama Samia ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa wilaya ya Iramba muda mfupi baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Kinampanda na maboresho na ukarabati wa chuo cha Ualimu Kinampanda pamoja na kiwanda kikubwa cha Yaza cha kukamua mafuta ya alizeti ambacho kinamilikiwa na Yusuph Nalompa mkazi wa Ndago,
Alisema serikali ya awamu ya tano inapenda kuona wazawa wakinufaika zaidi na rasilimali mbalimbali ikiwemo madini. “Kwa maoni yangu napendekeza maeneo ambayo leseni zake zimefutwa, wapewe vijana wachimbe na Mapato watakayopata, wahakikishe wanalipa kodi stahiki na kwa wakati ili serikali iweze kugharamia miradi ya maendeleo ya wananchi” alisisitiza Mhe: Mama Samia.
Katika hatua nyingine, Mhe: Mama Samia amewataka wakazi Iramba Mkoa wa Singida, wenye sifa za kupiga kura, wajitokeze kwa wingi kuchangua viongozi wa serikali za mitaa watakaoendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano. “Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu, utumike kuchangua viongozi wenye uwezo wa kufanya kazi na kwenda haraka na sera za serikali kusimamia miradi yetu na kutuletea maendeleo. Wawe ni watu madhubuti ndani ya mioyo yao, wawe na uzalendo wa kweli. Tukichangua viongozi bora, tutakuwa tumeweka msingi mzuri na imara kwa ajili ya uchanguzi mkuu utakaofanyika mwakani”alisisitiza Mhe: Mama Samia.
Aliongeza kusema, Tuhakikishe kituo cha afya cha Kinampanda kinamalizika ili serikali ilete Watumishi, vifaa tiba pamoja na dawa ili wananchi waweze kupata huduma. Hatuna changamoto ya Dawa, vifaa tiba wala Watumishi. itategemea na sipidi yenu ya kumaliza ujenzi wa kituo cha afya cha Kinampanda alisisitiza Mhe: mama Samia
Kuhusu gonjwa la UKIMWI, Makamu wa Rais, alisema mkoa wa Singida hauko vizuri katika maambukizi ya VVU, kwa madai kuwa maambukizi kwa sasa ni asilimia 3.6 ambapo miaka ya nyuma ilikuwa asilimia 3.1. “Taarifa nilizonazo ni kwamba wanaume wa mkoa huu, sasa wanakimbilia zaidi wasichana wenye umri mdogo kwa imani kwamba hawajaambukizwa UKIMWI. Hawawakimbilii wanawake wenye umri mkubwa, wakiamini kuwa wengi wao hawapo salama, alisema Mhe: Mama Samia “Kwa ujumla nitoe onyo kwamba UKIMWI bado hauna chanjo wala tiba, kila mtu achukue tahadhara na gonjwa hili baya”.
Serikali imekuja na mpango wa sheria ya Bima ya afya ambapo kila Mtanzania anatakiwa kuwa na bima ya afya. Kila mtanzania anatakiwa kuwa na Bima ya afya na itatolewa kwa gharama nafuu, hii ni kwasababu kila mtanzania aweze kutibiwa kwa gharama nafuu sana na malazi yanapokuja hayakupi taarifa lakini ukiwa na bima ya afya utapata huduma kwa gharama nafuu alisisitza Mhe: mama Samia.
Akizungumza juu ya kumaliza changamoto ya maji wilayani Iramba, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe: Mama Samia Suluhu Hassan amesama Mradi wa uchimbaji wa visima 3 vya maji kata ya Mgongo, tunategemea baada ya uchimbaji wa visima hivi kukamilika vitakuwa na uwezo wa kutoa takribani lita milioni 2.1 kwa siku. Nia ya serikali ni kuhakikisha watanzania wote wanapata maji safi na salama na ifika mwaka 2020 vijiji vyote Tanzania vitapata maji safi na salama kwa asilimia 85 na maeneo ya mijini yatapata maji kwa asilimia 100 alisema Mhe: Mama Samia.
Aliongeza kusema “kuna mradi mwingine wa maji unatokea ziwa victoria kuleta maji Tabora, Igunga na Tarafa ya Shelui ambao utagawa maji katika vijiji vyote vya Shelui ili kuhakikisha watanzania wanapata maji safi na salama.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe: Mama Samia alisema umeme ufungwe Kijiji kwa Kijiji, Kitongoji kwa Kitongoji, Nyumba kwa Nyumba bila kuruka nyumba yoyote, Wananchi wote wafungiwe umeme kwa elfu 20000 na kila kijiji kipate umeme wilayani Iramba. alisisitiza Mhe. Mama Samia.
Ameagiza Halmashauri ya wilaya ya Iramba kuhakikisha inapeleka fedha zilizotengwa kwa ajili ya Vijana na wanawake. “Uwezeshaji wa vijana na wanawake lazima ufanyike. Hizi fedha zinatengwa kwa ajili ya kuwezesha vijana na wanawake, hii ni haki yenu, Vijana lazima mdai hizi fedha kutoka Halmashauri kwa sababu ni haki yenu.
Vile Vile amewashauri kuacha kukata miti ili kuwa na mazingira bora. Amewaasa wananchi katika wilaya ya Iramba kutunza mazingira, Kupata mvua ya kutosha pia kuifadhi mfumo wa maji kwa maendeleo ya jamii “Naomba mujitahidi kupanda miti ili turudishe hali nzuri ya ya hali ya hewa. Mtunze mistu kwani ndo uhai wetu, tunza mazingira ili mazingira yatutunze” Alisisitiza Mhe: Mama Samia
Amemwagiza Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula kuhakikisha anasimamia migogoro ya ardhi, amewataka Viongozi ngazi ya wilaya, tarafa, kata na kijiji kushirikiana kutatua migogoro ya wananchi. “hatutaki kusikia wananchi wamepigana, wamejinyonga kwasababu ya migogoro ya ardhi alisisitiza Mhe:Mama Samia
Wakati huo huo, Waziri wa Madini, Mhe: Dotto Biteko, alitumia mkutano huo kutoa onyo kwa watu ambao wanadhani sekta ya madini bado ni mahali pa kuchezea, watakuwa wanakosea sana. “Sasa hivi tumejipanga vizuri kuhakikisha Madini yananufaisha Watanzania na si vinginevyo. Tumechezewa sana, watu ambao si wazawa, wamenufaika mno na madini yetu. Matarajio yetu sasa, ni Watanzania kunufaika. Tuna uhakika huo, kutokana na serikali ya awamu ya tano, imekutunga sheria mpya ambazo hazitoi nafasi kunufaisha watu kutoka nje ya nchi” alisema Mhe: Biteko
Mbunge wa jimbo la Iramba, Mhe: Dkt. Mwigulu Nchemba ameishukuru serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe: Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa shillingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya Ndago na Kinampanda na Gari la kubebea wagonjwa.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.