Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amekabidhi pikipiki nne kwa Maafisa Tarafa wa Tarafa ya Kinampanda, Kisiriri, Ndago na Shelui.
Makabidhiano hayo ameyafanya leo Ijumaa Machi 20, 2020 mbele ya jengo la Mkuu wa Wilaya ya Iramba mjini hapa.
Luhahula amewaomba Maafisa Tarafa hao kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kuleta maendeleo na kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
“ Na sasa ninaamini mtafanya majukumu yenu kwa kasi zaidi, ninaomba mzitunze kwa kuwa ni mali ya Serikali japokuwa mmekabidhiwa nyinyi,” amesema Luhahula na kuongeza
“ Tuko katika kampeni ya kuzuia na kuelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa korona, tumieni pikipiki hizi kuzunguka katika maeneo yenu kuhakikisha wananchi wameweka maji ya kunawa na sababuni pamoja na dawa za kupaka.”
Amewaagiza Maafisa Tarafa hao kuhakikisha kuwa ofisi zote za umma na binafsi zinakuwa na vyombo vyenye maji na sabuni pamoja na kufuata maelekezo ya wataalam wa Afya.
“ Hakikisheni kuwa vifaa vya kunawia vimewekwa mpaka kwenye ofisi za watendaji wa vijiji ili kuilinda Iramba pamoja na Taifa letu,” amesema Luhahula
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu mbalimbali namna ya kujikinga na visuri vya korona kwa kufuata maelekezo ambayo yanatolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.
“Tunaendelea kutoa elimu ya kuzingatia usafi wa kila unapotoka kwenye tukio moja kwenda kwenye tukio lingine kunawa maji yanayo tiririka kwa sabuni na kuhakikisha wananchi wanaepuka mikusanyiko mikubwa kwenye maeneo mbalimbali,” amesama Mwageni
Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Pius Songoma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi ambayo aliwaahidi Maafisa Tarafa Nchi nzima kuwapatia vitendea kazi.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya pikipiki hizi ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ameitekeleza,” amesema Songoma
Akiongea katika makabidhiano hayo kwa niaba ya Maafisa Tarafa wa Wilaya ya Iramba, Mwenyekiti wa Maafisa Tarafa hao, Nicholas Mokoye amesema kuwa watatumia pikipiki hizo kuhamasisha na kufuatilia wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na virusi vya korona.
“ Sisi kuwa na pikipiki hizi ni faraja kwetu kwa kuwa tutaweza kufika maeneo yote na kufanya kazi zetu kuwa nyepesi na rahisi sana,” amesema Makoye
Amesema kuwa watatumia pikipiki hizo kutekeleza majukumu na kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika Tarafa zao.
MWISHO
Afisa Tarafa wa Tarafa ya Shelui, Nicholas Makoye akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi yake aliyowaahidi Maafisa Tarafa Nchi nzima wakati alipoongea nao Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Hemedi Munga
Fundi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Ndugu Matoto akizikagua pikipiki kabla ya kuzigawa kwa maafisa Tarafa wa Tarafa ya Kinampanda, Kisiriri, Ndago na Shelui. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.