Kutokana na mvua inayonyesha mfululizo Wilayani Iramba imeleta maafa makubwa katika familia ya mzee Athumani Daudi (miaka 84) Mkazi wa Kijiji cha Kisana Tarafa ya Kisiri wilayani Iramba ambaye amefariki Dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba ya udongo maarufu kama tembe walimokuwa wamelala usiku wa kuamkia leo.
Mke wa Marehemu Wintyapa Kitundu (miaka 79) amenusurika baada ya kupata majeraha ambapo amelazwa katika Hospitali ya wilaya Kiomboi Wilayani Iramba akipatiwa matibabu.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Mhe: Emmanuel Luhahula amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa kuanguka kwa nyumba hiyo kumetokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Akizungumza na Wananchi kwenye tukio amewataka wakazi wa wilaya ya Iramba kuchukua tahadhari kutokana na mvua inayoendelea kunyesha. Vilevile ameyasema hayo alipotembelea katika kata ya Kyengege kujionea namna mvua zilivyoleta madhara katika makazi ya watu.
Kutokana na athari ya mvua zinazoendelea kunyesha Wilayani Iramba na Kusababisha uharibifu wa Nyumba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula amewataka wakazi wote wa kata ya Kyengege walioathrika wahame maeneo hayo mara moja na kupewa eneo la kujihifadhi. Aidha ametoa wito kwa wakazi kukarabati nyumba zao na kujenga nyingine za kudumu ili kuepuka maafa ya kuangukiwa na nyumba za tembe yanayotokea mara kwa mara.
Picha ikionesha nyumba ya udongo maarufu kama tembe iliyoanguka kutokana na athari za mvua zinazoendela kunyesha Wilayani Iramba.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.