Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Baraza la Madiwani wilayani Iramba Mkoa wa Singida limepitisha takribani Tsh 41.163 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mipango ya maendeleo kutoka kwenye vyanzo vya Halmashauri, Ruzuku ya Serikali, Wahisani na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Baraza la Madiwani limepitisha bajeti hiyo leo Februari 22, 2022 katika kikao cha mapendekezo ya makasio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano mjini hapa.
Akiongea katika Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Innocent Msengi aliwataka Madiwani kwa kushirikiana na Wakuu wa Idara na Vitengo kutambua kuwa bajeti hiyo itafikiwa ikiwa watadumisha ushirikiano wa kusimamia ukusanyaji wa mapato.
“ Niwaombe sana Madiwani na Wakuu wa Idara kutambua kuwa mzigo huu wa kukusanya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hii ni wetu, hivyo tujitoe kwa dhati ili Iramba iendelee kuhudumia wananchi wake kwa weledi wa hali ya juu.” Alisema
Bajeti hii imekuwa ya mfano ukilinganisha na bajeti iliyopita ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ilikisia kukusanya takribani Tsh 34.174 bilioni wakati mwaka wa fedha 2022/2023 ikikisia kukusanya takribani Tsh 41.163 bilioni.
Akitoa salamu za Serikali mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda aliwakumbusha Madiwani pamoja na Wataalamu wote kuhakikisha maadalizi ya Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2022 yanafanyika kwa weledi mkubwa ili kufanikisha azma ya serikali ya kutoa huduma kwa wananchi kikamilifu.
Mwenda alifafanua kuwa Sensa ya Watu na Makazi itasaidia kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kuiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi wake.
Aidha, alisema kuwa zoezi hili litakuwa na faida kubwa kwa nchi na raia wake kutambua idadi ya watu na makazi yao, hivyo ni rahisi serikali kupanga bajeti ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kulingana na mahitaji ya jamii katika kila eneo.
Halikadhalika, aliwataka Madiwani kwa kushirikiana na Wataalamu kutekeleza agizo la serikali la upangaji wa postikodi kwa ajili ya anuani za makazi kwa sababu kutarahisisha mawasiliano na utoaji wa huduma za msingi kwa wanawake.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Michael Matomora aliwashukuru wadau wote kwa namna walivyoshirikiana kufanikisha rasimu ya bajati ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Aidha, amewaomba wajumbe hao kufahamu kuwa watatumia fedha kufuatia mipango iliyopo katika bajeti ambayo wameipitisha.
“Niwashukuru wadau wote kwa kushiriki kuandaa rasimu ya bajeti na kutoa wito kuwa mchakato huu ni endelevu bado tunaendelea kupokea maelekezo ya serikali kwa namna ambavyo itaona inafaa.” Alisisitiza
Aidha, alibanisha kuwa katika suala la kukusanya fedha haitarajiwi mkusanyaji fedha kupendwa na kila mtu, hivyo endapo Madiwani watasikia malalamiko basi wayapokea kwa mtazamo chanya kwa lengo la kukusanya fedha tu, kwa sababu fedha pekee ndio inapendwa na kila mtu.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mtekente wilayani humo, Nowel Shole alichangia katika bajeti hiyo kuongeza umakini na usimamizi katika mazao ya misitu kukusanya mapato ili kuhakisha bajeti hii inatekelezeka.
Iramba imekuwa na misitu ya hifadhi mingi ambapo hapo awali walikuwa hawakusanyi ushuru, hivyo katika bajeti hii waingizaji wa mifugo na watakaokamatwa katika uchomaji na uuzaji wa mkaa watatozwa ushuru.
Naye Albert Makala Diwani wa kata ya Mtwike wilayani humo alisema kuwa katika bajeti hii kunaongezeko la takribani asilimia 26 ukilinganisha na bajeti ya mwaka jana, hivyo aliiomba Halmashauri ijikite kutekeleza miradi ya maendeleo na kuhakikisha miondombinu ya barabara inapewa kipaombele ili kurahisisha mawasiliano ambayo yatachochea shughuli za uchumi.
Baraza la Madiwani limepitisha rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 hivyo limehitimsha mchakato wa rasimu hiyo na kusubiria Baraka za Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.