Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Baraza maalum la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida limepitisha rasimu ya bajeti ya kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 38.6 kwa mwaka wa fedha mwaka 2020 / 2021.
Baraza hilo limepitisha rasimu hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
Jumla ya Tsh38.47 bilioni zimepitishwa kutoka serikali kuu, Wadau mbalimbali wa Maendeleo na Makusanyo ya Halmashauri ambayo yamekadiriwa kukusanywa na kutumiwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Rasimu hiyo imeongezeka kwa mwaka wa fedha 2020/2021ukilinganisha na bajeti iliyopitishwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo Tsh27.15 bilioni zilikadiriwa kukusanywa na kutumika toka serikali kuu, Wadau wa Maendeleo na Makusanyo ya Halmashauri.
Awali akiwasilisha rasimu hiyo Kaimu Afisa Mipango, wa Halmashauri hiyo Emmanuel Migunga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmahauri hiyo, Linno Mwageni amesema katika fedha hizo bilioni Tsh32,755,926,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi , bilioni 2,099,859,499 kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi, bilioni 3, 658,801,592 miradi ya maendeleo na milioni 110,000,000 kwa ajili ya michango ya jamii.
Halmashauri hiyo ipo kwenye mwaka wa watano wa kutekeleza mpango mkakati kwa kipindi cha miaka mitano ya awali ya utawala wa awamu ya tano ulioanzia mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2020/2021.
‘’ Maandalizi ya mpango huo yamezingatia mpango wa maendeleo wa Dunia, mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, Ilani ya uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015, Muongozo wa bajeti toka Wizara ya fedha, Muongozo wa Wizara ya TAMISEMI, Maelekezo ya Mkoa, Maelekezo ya Wizara mbalimbali kama Kilimo, Maji, Elimu, Afya, Utumishi na Mifugo. ’’ amesema Migunga
‘’Mpango huo umejikita kutekeleza dira ya Halmashauri kuwa na jamii yenye maisha bora na maendeleo endelevu na kutimiza dhima ya kutoa huduma bora kwa jamii kwa kutumia vizuri rasilimali, kujenga uwezo na utawala wa kisheria ili kuwa na maisha bora’’amesema.
Migunga amesema katika taarifa hiyo kuwa Halmashauri hiyo inahakikisha malengo ya kupambana na janga la ukimwi, kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kupambana na rushwa, kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi vinatimia.
Pia kuongeza idadi na ubora wa huduma za jamii na miundombinu, kusimamia utawala bora wa kisheria,
kuboresha ustawi wa jamii, jinsia na uwezweshwaji wa jamii, kukabiliana na dharura na maafa ili kuwezesha jamii kushirikiana katika kupanga na kutekeleza vipaumbele vyake na kuboresha masuala ya Lishe hasa kwa watoto umri chini ya miaka mitano.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Tyosela amewahimiza Madiwani kusimamia mapato ili kuipeleka Halmashauri katika muelekeo unaotakiwa kusimamia shughuli za maendeleo.
Pia itasababisha huduma za kijamii kupitia mapato ya ndani kuweza kupatikana kila kata.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni ametoa taarifa kwa Madiwani wa Halmashauri hiyo kuhusu fedha iliyototewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliposimama kwa muda kuwasalimia wananchi wa Shelui na kuwaunga mkono kwa kutoa kiasi cha Tsh milioni 250 za kituo cha Afya cha kata hiyo, lakini badala yake ametoa shilingi milioni 400.
Mwageni alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wananchi wake kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya huduma ya Afya hivyo aliwasihi Madiwani hao kumuunga mkono kusimamia miundombinu inayotolewa na serikali ili wananchi wapate huduma stahiki.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Simion Tyosela amewahimiza Madiwani kusimamia mapato yatakayoiwezesha Halmashuri kwenda katika muelekeo unaotakiwa wa kusimamia shughuli za maendeleo. Kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Samwel Shillah na Kulia mwa Mwenyekiti ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni amewaambia Madiwani kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameleta Tsh400 milioni kwa ajili ya kituo cha Afya Shelui na TAMISEMI imewapatia POS 43 (point of Sel) za kukusanyia mapato. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya Wakuu wa Idara mbalimbali wakifuatilia upitishaji wa rasimu ya mpango wa kati na makisio ya bajeti ya mwaka 2020 hadi 2021. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.