Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani amerasimisha tukio la kwanza la uchorangaji kwa ajili ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Dkt, Kalemani amelifanya zoezi hilo mwishoni mwa wiki hii wakati alipofanya ziara katika Bonde la Eyasi Wembere kijiji cha Luono Wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
“Sasa tunaanza safari ya kwenda kupata mafuta ambapo kwa hatua tuliyofikia inatoa matumaini kuwa tunayo miaka miwili toka sasa tunaweza kugundua mafuta ambayo ni neema kubwa sana,” amesema Dkt, Kalemani na kuongeza kuwa
“Shughuli za utafiti wa mafuta zinaendelea katika maeneo mengine ya Tanga kasikazini, Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa na Bonde la Eyasi Wembere ambapo eneo hili la Wembere limeonesha kwa hatua ya haraka uwepo wa mafuta ya kuchimba.
Katika hatua hiyo amempongeza Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli katika awamu yake imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya utafutaji na uchorongaji wa mafuta na gesi asilia Tanzania.
“Ndugu zangu tambueni kuwa mwaka jana tulitenga fedha kwa ajili ya utafutaji na uchorongaji wa kuelekea kuchimba mafuta takribani dola 500milioni serikali imetoa” amesema na kutolea taarifa kuwa
“Kwa sasa tunamafuta yaliopo chini bado hayajakuja juu, hivyo tunaendelea kuyatafuta ili tuyatumie na kilichokuja juu ni gesi asilia ambayo tayari tunayo takribani 57.5 trilioni za gesi,”
Amefafanua kuwa tukio hilo la uchorongaji katika Bonde la Eyasi Wembere ni tukio kubwa kwa kuwa ndio tukio la kwanza la uchorongaji na utafutaji wa mafuta Nchini, hivyo ni bahati kwa wananachi wa Luono na Iramba kushuhudia tukio kubwa ambalo halijawahi fanyika sehemu yoyote Tanzania.
Akitoa taarifa fupi ya utafutaji na uchorongaji wa mafuta na gesi asilia katika Bonde la Eyasi Wembere Nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta la Taifa TPDC, Dkt. Vames Mataragio amesema kuwa wanalo jukumu la utafuatiji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi.
“Mhe, Waziri tayari tumechimba visima 3 vyenye umbali wa mita 300 kwa lengo la kupata miamba tabaka yenye mafuta ilivyoenea ili kuweza kupata mafuta na gesi asilia,” amesema Dkt, Mataragio
Pia ameongeza kuwa wanaona upo uwezekano mkubwa wa kuwa na mafuta na gesi asilia kwa sababu jirani zetu Kenya na Uganda tayari wameisha pata mafuta katika maeneo ambayo yanafanana kabisa na maeneo ya Bonde la Eyasi Wembere.
“Mhe, Waziri hadi kufikia hapa tumeishatumia 7.6 bilioni katika utafiti ambapo 7.3bilioni zilitumika katika uchukuaji wa data kwa kutumia ndege huku 300milioni zikitumika kuchoronga visima vitatu,” amefafanua Dkt, Mataragio
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amewashukuru wananchi wa Luono wa Bonde la Eyasi Wembere kwa kudumisha ushirikiano na usalama wa Uchorongaji na utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwani mafuta yakipatikana yataweza kuwanufaisha wananchi wa Luono, Iramba, Singida na Tanzania kwa ujumla.
Naye Mkazi wa Kijiji cha Luono, Emmanuel Gedenga ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta mradi huo katika Kijiji cha Luona kwa sababu ikiwa mafuta yatapatikana wataweza kupata ajira za kutosha na kukifanya kijiji chao kuwa kama Ulaya.
Ufuatiliaji wa mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere ulianza mnamo mwaka 2015/2016 kwa TPDC kufuatilia taarifa za awali za Kijiofizia za Nguvu za Uvutano na Usumaku ambazo zilionesha uwepo wa kina kirefu cha miamba tabaka yenye kuzalisha mafuta na gesi asilia.
MWISHO
Mhandisi Koleta Selsi akitoa maalezo ya hatua ya uchorongaji wa visima vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia ilipofikia mbele ya Waziri wa Nishati, Medard Kalemani alipofanya ziara katika kijiji cha Luono Bonde la Eyasi Wembere julai 23, 2020. Picha na Hemedi Munga
Mtambo unaotumika kuchorongea visima vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia Kijiji cha Luono Bonde la Eyasi Wembere Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Huo ndio Mtambo unaotumika kuchorongea visima vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia Kijiji cha Luono Bonde la Eyasi Wembere Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya miamba tabaka iliyotoka katika visima vitatu vilivyochimbwa Kijiji cha Luono Bonde la Eyasi Wembere tayari kwa kupelekwa maabara kubaini uwepo wa mafuta na gesi asilia katika eneo hilo. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa TPDC. Kulia mwa Waziri huyo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Zainab Said na Kushoto mwa Waziri huyo ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa TPDC. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.