Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Bishop Robert Kijanga wa kanisa la Evangelistic Assemblies of God Mjini Kiomboi amewaongoza Wachungaji katika maombi ya kupunguza ajali maeneo ya Kizonzo na Mgongoro yaliopo barabara kuu itokayo Singida kuelekea Jijini Mwanza.
Maombi hayo yamefanyika leo Ijumaa Aprili 3, 2020 katika maeneo tofauti tofauti ya barabara hiyo kuanzia Mgongoro hadi eneo la daraja la Sekenke chini ya Mlima Sekenke.
Akiongea katika maombi hayo, Bishop Kijanga amesema kuwa barabara hiyo imetengenezwa ili watu wapitishe mizigo ya biaashara, kurahisisha usafiri na sio barabara ya mauti au kufanyiwa ibada za kishetani.
“ Mungu anayo haki ya kushinda, hivyo nia yetu ni kuvunja roho, mkuu wa anga atoae roho za watu mahala hapa, kuvunja nguvu za giza na vile vyote vinavyoingilia maisha na kuharibu mfumo wa binaadam,” amesema Bishop Kijanga na kuongeza
“ Tunamuomba Mungu kuleta usalama na amani katika barabara hiyo, kijiji cha kizonzo, kijiji cha Mgongoro na abiria wote wapitao katika barabara hiyo.”
Halikadhalika, amesema kuwa maandiko matakatifu yamesema kuwa mchawi hapaswi kuishi haswa anapokataa maandiko matakatifu yasemayo kuwa ombeni mtapewa, tafuteni mtaona, bisheni mtafunguliwa na andiko lisemalo niite nami nitaitika nami nitakuonesha mambo makubwa magumu usiyoyajua na maandiko mengineyo.
Kwa upande wake Mchungaji Robert Lugiko ameombea maeneo hayo kuvunja nguvu za kichawi na nguvu za giza ili pawe salama.
“ Na tunakwenda kukomesha ajali katika eneo hili, kufuta jini na ajenti mkuu kutoka kuzimu mwenye kuangamiza roho za wanaadamu,” ameomba Lugiko
Mchungaji kutoka kitukutu, Yona Kidavya ameombea vyombo vya moto na madereva wake waepukane na vituko mbalimbali vya barabarani huku akikemea aina yoyote ya vitu vinavyoonekana na visivyoonekana vinavyosababisha utokeaji wa ajali.
Naye Afisa Tarafa wa Tarafa ya Shelui wa Wilaya hiyo, Nicholas Makoye amewashukuru Wachungaji hao kwa maombi ambayo huenda Mungu akanusuru roho za watu zinazopotea katika maeneo hayo kutokana na ajali za mara kwa mara.
Akitoa ushuhuda mmoja wa wakazi wa Kizonzo katika maombi hayo, Nkumbi Temwa amesema kuwa kutokana na yanayo zungumzwa na Madereva mbalimbali kuwa maeneo hayo hujitokeza mwanamke ambaye hajulikani maeneo anayoishi na punde baada ya kutoweka hutokea ajali.
“Hapa kuna pepo limeanza kusumbua na kusababisha ajali na huonekana binti ambaye hajulikani anakaa wapi na hafahamiki sura yake,” amesema Temwa
Naye mchungaji Samwel Majuta amesema kuwa wanaamini kuwa maombi walioyaomba Mungu ameyasikia na bila shaka atawajibu, hivyo ajali zote zitakoma katika maeneo hayo.
Maombi hayo yamefanyika kufuatia ajali iliyotokea wiki iliyopita ya lori lenye usajili namba T939 CBW lilipokuwa linalipita gari dogo (overtaking) na kugongana uso kwa uso na basi la MJ Safari lenye usajili namba T779 AWJ.
Kufuatia ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula alipotembelea eneo la ajali aliahidi kupeleka timu ya maombi kuombea kutokomeza ajali hizo.
Timu hiyo ya maombi, im emetembelea na kuomba takriban 38 kilometa za barabara hiyo kuanzia Malendi mpakani mwa Mkoa wa Singida na Tabora, Kizonzo, Shelui, Sekenke na Misigiri.
Maombi hayo yamejikita kuombea kuvunja roho zilizokalia Kizonzo na Mgogoro, kuombea madereva wote kuendesha vizuri kwa kuzingatia taratibu za barabara, kuombea barabara na mipaka yake kuwa salama, kuombea abiria wote wanaopanda magari kuwa salama, kuombea vyombo vya moto na kuombea Serikali ya Wilaya ya Iramba na Wasimamizi wa miundombinu ya Barabara.
MWISHO
Bishop Robert Kijanga akiombea barabara itokayo Singida kwenda Jijini Mwanza eneo la mpakani kati ya Wilaya ya Iramba na Igunga. Picha na Hemedi Munga
Mchungaji Samwel Majuta akiombea barabara itokayo Singida kuelekea Jijini Mwanza eneo la Kizonzo Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Mchungaji Yona Kidavya akiombea barabara itokayo Singida kuelekea Jijini Mwanza eneo la Malendi mpakani mwa Mkoa wa Singida na Tabora. Picha na Hemedi Munga
Afisa Tarafa wa Tarafa ya Shelui Wilayani Iramba, Nicholas Makoye akiwashukuru Wachungaji kwa maombi waliyoyaomba kwenye barabara itokayo Singida kuelekea Jijini Mwanza eneo la Malendi mpakani mwa Mkoa wa Singida na Tabora. Picha na Hemedi Munga
Bishop Robert Kijanga akiwa na wachungaji mbalimbali wakiombea barabara itokayo Singida kwenda Jijini Mwanza eneo la Kibigiri kata ya Shelui Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Bishop Robert Kijanga akiwa na wachungaji mbalimbali wakiombea barabara itokayo Singida kwenda Jijini Mwanza eneo la daraja la sekenke chini ya Mlima wa Sekenke Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.