Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Mhe. Suleiman Yussuf Mwenda ameiomba Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuendelea kutoa mafunzo ya kilimo hususani kanuni za kilimo bora kwa maafisa ugani na wakulima wilayani humo ili kuboresha kilimo na kuongeza tija katika mazao ya kilimo.
Mhe. Mwenda alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo (2021/2022) Kiomboi Wilayani Iramba Mkoani Singida ambapo wadau mbalimbali wa kilimo walishiriki katika uzinduzi huo wakiwemo Wizara ya Kilimo, Wakulima , Maafisa Ugani, Taasisi binafsi na za Serikali (TARI, NMB, Shirika la Posta, TANESCO, Bodi ya Pamba, Feed the future, Action Against Hunger, Bio Sustain, Reliance Group, ETG) pamoja na Makampuni ya mbegu (SUBA-Agro, DK, SeedCo, Kibo Seed).
Katika hotuba ya ufunguzi, Mheshimiwa Mwenda amesema TARI imekuwa ikitafiti mbegu bora za mazao mbalimbali na kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa maafisa ugani na wakulima hivyo kuitaka TARI kupeleka teknolojia hizo Wilayani Iramba ili wakulima waweze kunufaika kwa kulima kilimo chenye tija na kuachana na kilimo cha mazoea.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI aliyeshiriki katika uzinduzi huo Bibi Margaret Mchomvu alisema TARI imejipanga kupeleka teknolojia zilizoboreshwa Wilayani humo ikiwemo utoaji mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima kupitia mashamba darasa ambayo yataandaliwa wakati wa msimu wa 2021/2022 hasa kwa zao la alizeti.
Bibi Mchomvu aliongeza kuwa TARI pia imepanga kuandaa maonyesho makubwa ya teknolojia zake zote katika mnyororo wa thamani kwa lengo la kubadilisha mtazamo, fikra na kutoa elimu kwa wadau wa kilimo hasa kwa mazao ya alizeti, mahindi, mpunga, mtama, uwele, ulezi, pamba,mihogo, viazi vitamu, maharage na kunde. Mazao mengine ni ufuta, karanga, dengu, vitunguu na nyanya.
Nao baadhi ya Viongozi wa dini, Chama na Serikali walioshiriki katika uzinduzi huo wamewaomba wataalamu kilimo wawasaidie wakulima wilayani humo katika kuboresha na kubadilisha kilimo chao ili kiwe na tija na Iramba iwe na mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo.
Uzinduzi wa Msimu wa Kilimo Wilayani Iramba uliobebwa na kauli mbiu isemayo “Kilimo Iramba, Tija kwa kila mdau” ulifanyika Oktoba 6, 2021.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.