DC MWENDA AAGIZA USHIRIKI WA WAWEKEZAJI KATIKA MIRADI YA JAMII IRAMBA
Iramba, Singida – Mei 21, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Suleiman Yusuph Mwenda, ametoa agizo kwa serikali ya kijiji cha Nkokilangi kuhakikisha kuwa wawekezaji wote wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo wanashiriki kikamilifu kwenye programu za kurudisha kwa jamii (CSR), ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika moja kwa moja na uwekezaji unaofanyika kwenye ardhi yao.
DC Mwenda aliyasema hayo leo alipokutana na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Nkokilangi, kata ya Ntwike, kitongoji cha Kibululu Matanda. Lengo la kikao hicho likiwa ni kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wachimbaji hao katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
Katika kikao hicho, Mwenda alisisitiza serikali ya kijiji kuhakikisha inasimamia ipasavyo utekelezaji wa majukumu ya wawekezaji kwa jamii.
“Hakikisheni wawekezaji wote wa ndani na nje wanashiriki programu ya kurudisha kwa jamii lakini pia hakikisheni wananchi wote wa eneo hili wanapata taarifa zote muhimu juu ya uwekezaji huo. Wakija watuachie alama, alikuja Sunshine hapa akatuachia darasa Moja pale shule ya Msingi Nkokilangi. Tumieni muongozo kufahamu nini kinatakiwa kifanyike kwenye Jamii kwa kuzingatia uhitaji wa Jamii kwa wakati huu.” alisisitiza DC Mwenda
Mmoja wa wanakijiji, Michael Juma, alitumia nafasi hiyo kuwasilisha ombi kwa Mkuu wa Wilaya akiomba kutengwa kwa eneo maalum la kiwanja cha michezo kijijini hapo. Ambapo, Alisema kuwa kiwanja hicho kitakuwa msaada mkubwa katika kuendeleza shughuli za michezo na kujenga afya na mshikamano kwa vijana wa eneo hilo.
Katika hatua nyingine, DC Mwenda aliwataka wanakijiji wa Nkokilangi kujiandaa kwa ajili ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kufanya ziara Wilayani Iramba mwezi Julai 2025. Alisisitiza kuwa ni fursa ya kipekee kwa wananchi kuonyesha mshikamano na maendeleo ya Wilaya ya Iramba.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.