Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewaahidi wanafunzi kidato cha sita wanaotarajia kufanya mitihani yao Mei 9, 2022 endapo watapata matokeo mazuri kupata ufadhili wa masomo nchini China.
Mwenda ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Mei 08, 2022 punde baada ya viongozi wadini kuwaombea kidato cha sita wafanye vizuri katika mitihani yao, maombi hayo yamefanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Lulumba mjini Kiomboi.
Akiongea punde baada ya maombi hayo, Mkuu huyo wa wilaya aliwafahamisha wanafunzi hao kuwa maisha ya mafanikio kwao yanaanza katika hatua hiyo ya mtihani wa kidato cha sita.
Aidha, aliwataka kumtegemea Mungu kwa sababu yeye ndiye Muweza wa kila jambo.
“Pamoja na kujiandaa mlivyo jiandaa kimasomo bado ni muhimu kumtegemea Mwenyezi Mungu ambaye ndiye mlezi wetu, kiongozi wetu na mwenye maarifa ambaye kila mmoja wetu anamuomba na kumtegemea yeye.”
Hali hiyo ndio ilifanya viongozi wadini kufika shuleni Lulumba kwa ajili ya kufanya maombi maalumu kwa kidato cha sita, hivyo aliwaomba wanafunzi hao katika kipindi hichi kuzidisha ushirikiano na mshikamano wa kusaidiana kwa hali na mali.
Katika hali ya kuwapa motisha kama kichocheo cha wao kufanya vizuri katika mitihani yao, DC Mwenda alitoa ahadi ya ufadhili wa masomo nchini China.
“Mimi Mkuu wenu wa Wilaya ninaweka ahadi kwenu kwamba wanafunzi watatu watakaopata matokeo mazuri nitasimamia ufadhili wa masomo nchini China.” Aliahidi na kuongeza kuwa
“Ninapenda kuona wanafunzi waliosoma nchini China tunakuwa wengi.”
Awali akiongea katika hafla hiyo fupi Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo, Godfrey Mwanjala aliwaasa wanafunzi hao kuwa wanapaswa kujiamini pindi wawapo katika chumba cha mtihani kwa sababu wameandaliwa vizuri na wanaafya njema.
“Tuendelee kuomba kwa Mwenyezi Mungu muwe katika hali hii ya utimilifu ili muweze kufanya mitihani yenu mkiwa na afya njema.” Aliomba
Aidha, aliwasisitiza wanafunzi hao kuondoa hofu kwa sababu katika vichwa vyao wanauelewa wakutosha na maarifa ambayo wameyapata kutokana na maadili na malezi bora kutoka kwa walimu wao.
“Ndugu zangu wanafunzi kazi mlionayo sasa ni kufanya mitihani yenu kwa kutumia akili zenu na kuithibitishia hadhira ya watanzania kuwa ufaulu wenu ni wa halali kila mwaka.”
Akiwaombea dua wanafunzi hao Imamu wa Msikiti wa Taqwa mjini Kiomboi, Shekhe Ponda Rukumbwe alimuomba Mwenyezi Mungu kufawafanyia wepesi wanafunzi hao ili wavuke katika mitihani yao salama.
Rukumbwe alimuomba Mungu kuwafaulisha wanafunzi hao kama alivyo weza kumuokoa Nabii Musa (A.S) katika Bahari dhidi ya vitimbi vya Fir auni.
“Ewe Mwenyezi Mungu mwenye mamlaka ya wanafunzi hawa tunakuomba uwasimamie katika mitihani yao, uwaelekeze, uwafungulie, na uwaondeolea shaka huku ukiwafungulia pale palipo na uzito pawe pepesi hatimaye wafaulu wote.”
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Baptist wilayani hapa, Robert Lugiko aliwataka wanafunzi hao kukabidhi nafsi zao, maisha yao, mioyo yao, viti vyao na afya zao kwa Mungu Mtakatifu.
“Ewe Mtakatifu tunakuomba utoe kibali dhidi ya kalamu na madaftari haya uwabariki wanafunzi hawa ili waweze kufaulu.” Aliomba
Aidha, aliongeza kuomba kuwa Mungu tunakuomba uliweke anga hili salama na kuifanya Shule hii kuongoza katika Taifa.
Tunakuomba Mungu uwasaidie wanafunzi hawa waweze kufaulu wote.
Naye kaka Mkuu mstaafu wa shule ya Sekondari Lulumba, Kassimu Hassan alimuhakikishia Mkuu huyo wa wilaya kuwa watafanya vizuri katika mitihani yao ili kutengeneza maisha yao.
“Kwa kweli kwa namna ambavyo walimu wetu wametulea na kutufundisha vyema sisi tunasema tuko tayari kuifanya mitihani yetu na kwenda kulitumika Taifa letu.”
Halikadhalika, aliongeza kuwa matokeo watakayoyapata yatakuwa chachu ya walimu hao kupata nafasi mbalimbali za uongozi nchini.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.