Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Yusuph Mwenda ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Iramba kwa kupitisha bajeti ya makisio ya Mapato ya ndani ya kiasi cha Shilingi Bilioni 3.8 ikiwa ni ongezeko la bajeti hiyo ikililinganishwa na makisio hayo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ya Shilingi Bilioni 1.9.
Mwenda ameyasema hayo Februari 14, 2025 katika Baraza Maalumu la Madiwani kupitia na kupitisha makisio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Wilaya yetu inayo mafanikio makubwa sana katika utekelezaji wa bajeti zilizopita, tangu nimefika hapa kumekuwa na ongezeko la bajeti yetu na wakati wote tumekuwa tukiitekeleza kwa mafanikio. Tumeikuta bajeti ya Shilingi Bilion 1.2, leo kwenye baraza hili imepitishwa bajeti ya Bilioni 3.8, haya ni mafanikio makubwa sana.” Amesema DC Mwenda
Katika hatua nyingine Mwenda ametoa pongezi kwa wilaya ya Iramba kwa kushika nafasi ya 8 ikiwa na asilimia 13 kati ya kati ya Halmashauri 10 zilizoongeza ufaulu mtihani wa darasa la saba kitaifa wa mwaka 2024.
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Iramba likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Innocent Msengi limepitisha Makisio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya kiasi cha Shilingi Bilioni 38.08.
Bajeti ya Maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 imewasilishwa na Afisa Mipango Bw. Fadhil Hassan kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imekadiria kukusanya na kutumia Shilingi Bilioni 38.08 ambapo Ruzuku ya Mishahara Shilingi Bilioni 21.8, Ruzuku ya matumizi mengineyo Shilingi Bilioni 2.06, Mapato ya ndani shilingi Bilioni 3.8, Miradi ya Maendeleo 5.2 na Wahisani - Miradi ya maendeleo shilingi Bilioni 5.08.
Baraza la Madiwani limepongeza waandaaji wa Bajeti hiyo kwa kuzingatia vipaumbele mahususi vilivyowekwa Kwa ajili ya Maendeleo ya Halmashauri wakiamini Miradi ya Maendeleo itatekelezwa na Wananchi watapata huduma Stahiki.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.