Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amekemea tabia ya kujichukulia sheria mkononi kudhuru watu pindi inapokuwa imetokea kutoelewana kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya dhahabu na badala yake wafuate sheria, taratibu na kanuni katika kutatua migogoro inayowakabili.
Mwenda ametoa kalipio hilo leo Jumanne Aprili 5, 2022 wakati alipokuwa akiongea na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika mgondi wa Nabii Elia uliopo katika kijiji cha Misigiri kata ya Ulemo wilayani hapa.
“Ndugu zangu fahamuni kuwa jukumu langu lakwanza ni kuhakikisha hali ya usalama na amani kwa raia wote wilayani hapa.” Alisema
Aidha, aliwataka kuhafamu kuwa wao wametoka katika maeneo tofauti tofauti kuja kutafuta riziki katika mgodi huo, hivyo mgodi ukifungwa watapata shida katika kuendesha maisha yao.
Aliwaagiza wachimbaji hao kuwa na tabia ya kwenda polisi pale panapotokea mtu anatoa maneno ya kashfa, machafu na matusi ili polisi wamchukulie hatua na kuendelea nataraibu za kisheria.
“Hatuwezi kila mmoja awe anachukua sheria mkononi, kufanya hivyo ni kujiingiza katika makosa hata kama utakuwa ulichokozwa au haki ipo upande wako.” Alikataza
Kufuatia hali inayodaiwa kuwa baadhi ya viongozi na wachimbaji kupigana na kutiana majeraha, Mkuu huyo wa wilaya alikilani kitendo hicho nakuwataka wafahamu kuwa yeye akiwa Mkuu wa wilaya mwenye dhamana ya kulinda amani na usalama wa raia hajafurahia kitendo cha uvunjifu wa amani uliodaiwa kufanyika katika mgodi huo.
“Nakilani kitendo hichi, siridhiki na tabia hii, hivyo nawaasa ndugu zangu tufanye kazi hizi kwa kuzingatia na kuhesimu sheria, taratibu na kanuni ambazo serikali imeziweka.”
Akiongea na wachimbaji hao, Mkuu wa kituo cha Polisi kiliopo kata ya Ulemo wilayani hapa, Inspekta Alfred Mpimbwe aliwataka wachimbaji hao kuwa na nidhamu katika utendaji wa majukumu hayo na kufahamu kuwa pindi wanapokuwa wamepata fedha kutoka katika migao ya mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu husababisha mji wa Misigiri kuchangamka.
Awali akitoa taarifa fupi ya namna ambavyo ugonvi ulivyotokea mmiliki wa mgodi huo, Nabii Elia alimuomba Mkuu huyo wa wilaya kupiga marufuku Shimwaa (pombe) ambayo imekuwa ikisababisha vijana hao kulewa na hivyo kupoteza nguvu na kuwa chanzo cha ugonvi kwa wachimbaji.
“Kwa kweli chanzo kikubwa cha kukomesha migogoro na ugonvi migodini ni kupiga marufuku Shimwaa ambayo imekuwa ikiharibu vijana ambao ndio tengemeo la kujenga uchumi wa nchi yetu.” Aliomba Elia
Hata hivyo, wachimbaji wa madini ya dhahabu katika mgodi huo walitoa ushauri wa namna ya kutatua migogoro inayodaiwa kutokea katika maeneo ya migodi.
Kwa upande wake mmoja wa wachimbaji katika mgodi wa Nabii Elia, Saimon Kindago alishauri kuwa mmiliki wa mgodi huo abadilishe viongozi ambao wanasimamia shughuli mbalimbali katika mgodi huo kwa sababu ndio ambao wanadaiwa kuwa chanzo cha mgogoro huo.
Naye Francis Emmanuel alishauri kuwepo kitengo cha ulinzi na usalama katika mgodi huo ili kuhakikisha katika maeneo yote ya mgodi yanakuwa salama na pale panapowezakutokea mgogoro au uvunjifu wa amani wanawakamata wahusika na kuwafikisha katika mkondo wa sheria.
Akiongea na Mwandishi wetu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Dkt. Abel Mafuru alikiri kuwa mnamo Aprili 02 mwaka huu waliwapokewa majeruhi wawili ambao ni wakazi wa kijiji cha Misigiri wilayani hapa.
Dkt Mafuru alifafanua kuwa uchunguzi wa awali baada ya kuchukuliwa vipimo ulionesha kuwa Devison Samweli (56) alikuwa amevujika mfupa mkubwa wa mguu wake wa kulia na kuwa taratibu za kumpatia rufaa kwenda hospitali ya Mkoa wa Singida zinaendelea huku Peter Devis (37) akiwa amejeruhiwa katika paji lake la uso na kupata maumivu katika kifua chake.
Dkt Mafuru alithibitisha kuwa majeruhi hao hali zao zinaendelea vizuri.
Majeruhi hao wamedaiwa kupatikana kutokana na ugonvi ulioibuka katika mgodi wa Nabii Elia unaojishughulisha na kuchimba madini ya dhahabu.
Ilidaiwa kuwa chanzo kikubwa cha ugonvi huo ni ulevi uliopelekea wachimbaji hao kupigana baada ya kuchindwa kuelewana baada ya mchanga na mawe yanayodhaniwa kuwa yanadhahabu kupakiwa katika roli na kuonekana ujazo umezidi kiasi ukilinganisha na inavyokuwaga kwa ajili ya kuhamishwa kutoka duwara moja kwenda jingine.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.