Na Hemedi Munga
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amemuagiza Mkuu wa Polisi Tarafa ya Ndago INSP Rashidi Mchomvu kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wanaowatishia amani watumishi waliopangiwa majukumu ya kusimamia miradi ya maendeleo.
Mwenda ametoa agizo hilo leo Jumatatu Machi 28, 2022 wakati akiwa na Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Kamati ya Usalama wilaya kukagua miradi ya maendeleo katika kijiji cha Mwanduigembe wilayani hapa.
“Ninakupa wiki moja uhakikishe umewakamata watu wote wanaowatishia watumishi ambao wanatakiwa kusimamia miradi ya maendeleo ambao wanaogopa kudhuriwa na kuomba kuondoka katika kata ya Ndulungu na kuhamia kata nyingine.” Aliagiza
Aidha¸ aliongeza kuwa watu ambao wanaowatishia kuwadhuru watumishi wanatakiwa kufikishwa katika vyombo vya sheria ili watumishi hao waishi kwa amani na kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Alieleza kuwa haiwezekani apatikane mtu ambaye anazuwia miradi ya serikali isitekelezwe na kuwatishia watu kutopata amani wakati mimi nipo kwa ajili ya kuhakikisha amani ipo kwa watu wote.
Pia, aliwataka mafundi kuongeza kasi ya ujenzi kwa sababu wananchi wanayahitajia majengo hayo kwa kiu kubwa.
Alisisitiza ubora wa majengo hayo kuwa sawa na kiwango cha fedha takiribani Tsh 600 milioni zilizotolewa na serikali.
Katika hatua nyingia, Mkuu huyo wa wilaya alimuagiza Afisa Elimu Sekondari, Godfrey Mwanjala kuhakikisha atakapomuandikia Katibu tawala Mkoa wa Singida kuhusu fedha iliyobakia kutenga bweni la wasichana na wananume.
Halikadhalika, aliwataka viongozi wanaosimamia miradi hiyo kufanya kazi zao kwa uwazi ili kila mmoja awe anafahamu namna ambavyo fedha hizo zinavyotumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akiongea katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Iramba, Samwel Joel alieleza kuwa tayari watu wote wanaofanya wananchi wagome kujihusisha kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya maendeleo wamekwishachukuliwa hatua stahiki.
“Sisi tumeishamaliza kazi hasa kwa viongozi wote wanaofanya wananchi wagome na kukwamisha miradi tumeishawachukulia hatua zinazostahiki na suala hili limekwisha” alifafanua
Awali akitoa taarifa fupi mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Afisa Elimu Sekondari, Godfrey Mwanjala alisema kuwa wanatarajia kujenga madarasa manane na kuokoa baadhi ya fedha ambazo zinawezakutumika kujenga nyumba za walimu.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya! naomba kutoa taarifa kuwa hivi sasa Mhandisi anaandaa BOQ ya fedha ambazo tumeziokoa kwa ajili ya kujenga nyumba ya walimu baada ya kuomba kibali toka kwa Katibu Mkuu TAMISEMI.” Alisema
Kwa upande wake mmoja wa mafundi wanaojenga majengo ya madarasa hayo, Marcel Jacobo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea miradi ambayo imesaidia wao kupata ajira.
“Kwa kweli tunamshukuru Rais Samia na tunamuomba aendelee kuleta miradi mingine ili tupate ajira nakuweza kuendesha maisha yetu.”
Naye mmoja wa wanafunzi wa shule ya Sekondari Ndulungu, Swaumu Shila alimshukuru Rais Samia kwa kuwajengea shule kwani hapo awali hapakuwa na shule, hivyo walikuwa wakitembea umbali mrefu kuifuta shule ya Sekondari Mbelekese iliyopo katika kata ya jirani.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.