DC MWENDA AONGOZA HAFLA MAALUM YA KUWAAGA MADIWANI WA HALMASHAURI YA IRAMBA
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mkoani Singida, Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda, ameongoza hafla maalum ya kuwaaga Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba waliomaliza muda wao wa miaka mitano madarakani tangu walipochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hafla hiyo ya heshima imefanyika katika viwanja vya ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Juni 18, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi wa Dini, Serikali, pamoja na watumishi wa umma kutoka ofisi ya makao makuu ya wilaya hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mwenda aliwapongeza madiwani kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi chote cha uongozi wao. Alisema kuwa mchango wao umekuwa na matokeo chanya katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wa Iramba.
“Leo tumekutana hapa si tu kuwaaga viongozi wenzetu waliomaliza muda wao, bali kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya. Mmetuonyesha mfano wa utumishi wa umma uliojaa uwajibikaji, maadili, na uzalendo,” alisema DC Mwenda.
Aidha, Mhe. Mwenda aliwataka viongozi watakaochaguliwa baada yao kuendeleza misingi ya ushirikiano, uwazi, na kusikiliza wananchi katika kutekeleza miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mhe. Innocent Msengi ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kyengege amewashukuru wakuu wa ldara na Vitengo pamoja na wataalam wengine wa Halmashauri kwa ushirikiano hasa katika Usimamizi wa miradi ya maendeleo wilayani Iramba. Pia amewashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa ushirikiano wakati wote wa Uongozi wao katika Halmashauri hiyo.
Hafla hiyo iliambatana na utoaji wa vyeti vya pongezi kutambua mchango wa madiwani hao, ikiwa ni ishara ya heshima na shukrani kwa juhudi zao katika maendeleo ya Halmashauri.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.