Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Suleiman Mwenda Jumapili Disemba 8, 2024 amewaongoza Watumishi na wakazi wa kata ya Old Kiomboi kupanda miti katika Hospital ya Wilaya ya Iramba pamoja na Zahanati ya Tutu iliyopo kata ya Kiomboi wilayani humo, kuelekea maadhimisho ya kilele Cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambayo huadhimishwa Kila mwaka ifikapo Disemba 9.
DC Mwenda amesema Wilaya ya Iramba inasherekea maadhimisho hayo kwa kuwakumbusha Wananchi kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha wanaienzi amani ili nchi iendelee kubaki salama na kushiriki shughuli za maendeleo popote pale walipo.
"Moja ya jambo kubwa ambalo Kama taifa tunatakiwa kulienzi ni namna ya kuboresha, kuitunza na kuiendeleza amani ya nchi yetu. Ni tunu kubwa ambayo tuko nayo Kama taifa ambapo wenzetu maeneo mengi tunu hiyo hawana... Tunaposherekea uhuru wa Taifa letu lazima tujue kwamba tunao wajibu kama wananchi wa kushiriki shughuli za maendeleo popote pale ulipo. Maendeleo ya mtu mmoja mmoja ndio maendeleo ya Taifa." Amesema Mhe. Mwenda.
Pia Mwenda amesema katika kipindi Cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania bara Serikali kwa kushirikiana na Wananchi yapo mengi ya kujivunia kimaendeleo katika sekta mbali mbali kichumi kijamii na kitamaduni ikiwa ni matoke ya kupiga hatua katika maendeleo ya nchi.
"Wakati huo Wilaya nzima kulikuwa na sehemu tatu tu za kupata huduma za afya...Leo hii tunazungumza Kila Kijiji Kuna Zahanati, Kila kata ina Sekondari. Tuna sahemu zaidi ya 54 ambazo zinatoa huduma za afya katika Wilaya hii. Amesema DC Mwenda
Aidha DC Mwenda ametoa wito kwa Wananchi kuendelea na zoezi la upandaji miti katika Msimu huu wa mvua na kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili iendelee kukua kubaki salama.
Jumla ya miti 500 ya kivuli, miti ya mbao pamoja na miti ya Matunda imepandwa, katika zoezi la upandaji miti lilofanyika mapema leo Asubuhi kwenye maeneo mbalimbali Wilayani Iramba . Halmashauri ya Wilaya ya Iramba inaendelea kutekeleza agizo la Serikali la kila Halmashauri kuhaksikisha inapanda miti milioni moja na laki tano (1,500,000).
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.