Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida,Suleiman Yusuph Mwenda, amepongeza utekelezaji wa mradi wa uchimbaji visima vya umwagiliaji katika Kijiji cha Kyalosangi, unaotekelezwa kupitia Mpango wa Mifumo Himilivu ya Chakula kwa kuzingatia matokeo (TFSRP-PforR). Mradi huu, unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa gharama ya Shilingi milioni 187.7, unatarajiwa kunufaisha wakulima wapatao 200.
Akizungumza Februari 4, 2025, wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi eneo la mradi huo, DC Mwenda alisisitiza kuwa visima hivyo vitakuwa chachu ya maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji, hasa katika uzalishaji wa mboga na mazao mengine yanayohitaji maji ya kutosha.
"Mradi huu ni neema kubwa kwa wananchi wa Kyalosangi na Wilaya nzima ya Iramba. Nawasihi wananchi kushirikiana na wataalamu ili kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinatumika ipasavyo kwa maendeleo yenu," alisema Mwenda.
Pia aliishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji, akibainisha kuwa Wilaya ya Iramba ni miongoni mwa maeneo yanayonufaika na miradi hiyo katika Mkoa wa Singida.
"Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeweka mkakati madhubuti wa kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Hii inamaanisha kuwa sasa wakulima wa Iramba wataweza kulima mboga na mazao mengine kwa msimu wote wa mwaka, bila kutegemea mvua," aliongeza DC Mwenda.
Mradi huu ni moja kati ya miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji inayotekelezwa Singida, ikiwemo skimu ya umwagiliaji yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10, ambayo tayari inaendelea kujengwa. Miradi mingine itatekelezwa katika maeneo ya Kyengege, Ulemo, Mukulu, Old Kiomboi, na Mtoa.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.