DC MWENDA ASITISHA MKATABA WA UCHIMBAJI MADINI USIO NA MASLAHI BAINA YA USHIRIKA WA UKOMBOZI NA KAMPUNI YA GREAT DRAGON CO.LTD.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mkoani Singida, Suleiman Yusuph Mwenda, amevunja mkataba kati ya kampuni ya uchimbaji madini Great Dragon Co. Ltd na wanachama wa Ushirika wa Ukombozi kutokana na mapungufu yaliyobainika katika mkataba huo.
Uamzi huo umefanyika Machi 12, 2025 kijiji Cha Nkonkilangi kata ya Ntwike wakati wa kikao kati ya wanachama wa Ushirika wa Ukombozi na mwekezaji wa Great Dragon Co. Ltd. ambapo ilibaininika kuwa baadhi ya wanachama waliingia mkataba kinyemela na mwekezaji huyo kwa lengo la kumkabidhi sehemu ya eneo la leseni wanayomilikiwa na chama hicho, bila ridhaa ya wanachama wote.
"Mkataba huu una mapungufu mengi sana, lazima tuhakikishe tunaingia mikataba kwa maslahi ya pande zote mbili ili pande zote zinufaike." Alisema DC Mwenda.
Pia, Mwenda amewataka wanachama wa Ushirika huo kuhakikisha wanaingia mikataba yenye manufaa kwa wote na kufuata ushauri wa wataalamu wa sheria wakati wote wanapofanya maamuzi ya kusaini mikataba.
"Mikataba tunayoiingia lazima ilinde maslahi ya Ushirika wetu. Kila jambo tunalofanya, ni lazima tushirikishe wataalamu wa sheria kwa msaada zaidi." alisisitiza DC Mwenda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ushirika huo, Samike Soli, alibainisha kuwa alipoingia madarakani Novemba 2024, alikuta baadhi ya wanachama wakiwa tayari wamesaini mkataba na Great Dragon Co. Ltd bila kufuata taratibu sahihi.
Naye Paulo Emanuel Ulaya mmoja wa wanachama wa Ushirika wa Ukombozi alieleza kuwa mkataba uliosainiwa haukuwa sawa na makubaliano ya awali ya wanachama.
"Tulikubaliana tumpe mwekezaji maduara matatu tu, lakini wenzetu waliingia mkataba wa eneo lote bila wanachama kufahamishwa." Alisema Paulo Ulaya.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.