Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Suleiman Yusuph Mwenda ametoa onyo kwa watu binafsi wanaouza mbegu za ruzuku kwa wakulima bei tofauti na bei elekezi inayotambuliwa na serikali.
Mwenda amebainisha hayo 11/11/ 2024 baada ya kutembelea duka la wakala (Ongeza Agrovet Iramba) anayeuza mbegu za ruzuku kwa wakulima kwa bei rasmi wilayani humo na kujionea zoezi la uuzaji mbegu za ruzuku linavyoendelea, huku akiwataka wakulima kuhakikisha wananunua mbegu kwa wakala aliyethibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI).
“Lazima tuchukue tahadhari na ndio maana tunaelekeza ili wananchi wetu wasipate hasara, maana mwisho wa siku mtu atanunua ataenda kupanda hekali kadhaa hamna kitu atanufaika nacho, akitoka pale atakuwa na malalamiko kwa sababu amenunua mbegu bandia. Lakini Tukiwaelekeza kwenye vituo maalumu hivi maana yake hata sisi serikali tumejiridhisha kwamba hilo ni zao lenyewe halisi.” Amesema Mwenda
Aidha amewataka wakulima kuhakikisha wanahuisha taarifa zao kwenye mfumo kupitia kwa maafisa kilimo waliopo katika kata na vijiji vyao, ili kupata namba ya mkulima na taarifa hizo ziendane na uhitaji halisi wa kiwango cha mbegu wanazohitaji kulingana na ukubwa wa mashamba yatakayolimwa msimu huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Iramba Bi. Marietha Kasongo amesema wanatekeleza agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mbegu zote za mahindi zinaingia kwenye ruzuku.
“Tuna kaya 51,000 ambapo kila kaya angalau wanapaswa kulima ekari tatu, na zote zilimwe kwa kutumia mbegu bora na mbolea za ruzuku…kwa hiyo tunahitaji kilo 1,241,184 za mahindi ambazo ni mbegu bora” Alisema Kasongo.
Katika hatua nyingine Bi. Kasongo ameipongeza kampuni ya Ongeza Agrovet kwa kuendelea na usambazaji wa mbolea za ruzuku. Na amewaasa wakulima ambao bado hawajashiriki katika zoezi la upimaji wa afya ya udongo kuhakikisha wanashiriki zoezi hilo kupitia kwa maafisa kilimo.
Hatua hii inajiri wakati ambapo tayari msimu wa kilimo kwa mwaka 2024/2025 ukiwa umezinduliwa rasmi kimkoa novemba mosi mwaka huu wilayani Iramba.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.