Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewataka watumishi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa inawajali na kuwathamini watumishi muda wote.
Mwenda ametoa wito huo leo Alhamisi Aprili 28, 2022 wakati wa hafla fupi ya mahafali ya kidato cha sita ya shule ya Sekondari Lulumba yaliofanyika katika viwanja vya shule hiyo wilayani hapa.
Ndugu zangu walimu naomba niendelee kuwatia moyo na kuwaaminisha kuwa serikali yenu inawajali, kuwathamini na kuitikia kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wakiwemo walimu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan siku chache zijazo tarehe moja kutoka leo tarehe 28 anakwenda kutamka jambo, hivyo mkae mkao wa kula ndugu zangu watumishi.” Alisema
Aidha, aliongeza kuwa Rais Samia akishirikiana na viongozi wengine serikalini wamekuwa wanawajali, wanawaheshimu, wanawathamini watumishi na kuwa imejiandaa kikamilifu kuendelea kutatua changamoto za watumishi.
Haya yanakuja ikiwa ni imani tuliyonayo kwa Rais wetu ambaye ni mwenye maono makubwa ya kuliongoza Taifa letu.
“Ni Rais bora, mchapakazi, mnyenyekevu, kiongozi mwenye utu na maono ya kuliongoza Taifa, hivyo tunaowajibu wa kumuunga mkono na kumpa ushirikiano.”
Akijubu risala ya wanafunzi kuhusu changamoto ya maji katika shule hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliiagiza Mamlaka ya maji ya Mji wa Kiomboi (KIUWSA) kuhakikisha kuwa maji yanatoka katika shule hiyo masaa 24.
Pia, aliwafunda wahitimu hao, kuendelea kuwa na nidhamu ya maisha ambayo humpelekea mtu kuwa na mafanikio kwa kuhakikisha wanakuwa na heshima, kujituma kwa juhudi na tabia njema wakati wote.
Halikadhalika, aliwasisitiza wahitimu hao kuendelea kudumisha upendo, uzalendo kwa Taifa na kuhakikisha watu wanapata mafanikio kupitia wao huku wakiendelea kusimamia mawazo yao ya mafanikio.
“Naomba niwaase ndugu wahitimu wakati wote elimu zenu na vipato vyenu wekeni kando pindi mnaposhirikiana na watu kuweni na haiba njema mtaishi maisha marefu sana.”
Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Muungano kufikisha miaka 58, Mwenda aliwataka wahitimu hao kuwa wazalendo kwa sababu Taifa linawategemea katika nyanja mbalimbali.
“Mimi nikiwatazameni naona Taifa lenye nguvu siku zijazo kwa sababu tunapata madaktari, wahandisi, walimu, wakuu wa wilaya na viongozi bora kutoka kwenu, hivyo jiandaeni kuwa watumishi wataifa hili.” Aliwaasa
Nilazima mtunze mshikamano na amani ya watu wa Taifa hili na kuhakikisha mnajituma huku mkikataa mawazo yenye kulifarakisha Taifa kwa mawazo ya kiukanda, kidini na ukabila.
Halikadhalika, aliwashukuru walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kufaulisha nakuifanya Iramba kuwa yakwanza kimkoa na hivyo kuwataka kuelekeza nguvu kuwa wakwanza kanda ya kati inayokusanya Mkoa wa Dodoma, Singida na Tabora ambapo ndani ya mikoa hiyo kunashule kongwe ambazo huingia kumi bora mara kwa mara.
“Tumekuwa wakwanza kimkoa lakini kuendelea kuilinda nafasi hii inahitajika juhudi kubwa na jitihanda za kutosha, hivyo niendelee kuwaomba ndugu zangu walimu kuwa tunalo deni la kuendelea kulinda nafasi hii na kuhakikisha tunaingia kumi bora katika mitihani ijayo.” Alisema Mwenda
Aidha, aliongeza kuwa wao wakiwa viongozi wilayani hapo wanatembea kifua mbele kwa matokeo mazuri ya Sekondari ya Lulumba.
Awali akiongea katika hafla hiyo mkuu wa shule hiyo, Jeremia Kitiku alisema kuwa wanaimani kuwa wanafunzi hao watafanya vizuri kuliko matokeo ya mwaka jana.
“Nitowe wito kwa wazazi wanotarajia kuleta watoto hapa kufahamu kuwa tunawandaa wanafunzi kufaulu kwa daraja la kwanza tu.” Alisema
Aidha, alisema kuwa ufaulo huo uliifanya shule hiyo mwaka 2020 kushika nafasi yakwaza kimkoa kati ya shule 15 na kitaifa 23 kati ya shule 586 huku mwaka 2021 ikishika nafasi yakwanza kimkoa kati ya shule 15 na kitaifa 24 kati ya shule 610.
Pia, alibainisha kuwa yapo masomo ambayo yaliweza kuingia kumi bora kitaifa ambayo ni Fizikia ikishika nafasi ya 5 kitaifa kati ya shule 462, Geografia ya 7 kati ya shule 750, Biolojia ya 17 kati ya shule 541, Kemia ya 12 kati ya shule 557, GS ya 13 kati ya shule 800, Hesabu ya 14 kati ya shule 435 na Bam ya 14 kati ya shule 624.
Halikadhalika, alieleza kuwa kwa upande wa masomo ngazi ya mkoa Lulumba ilishika nafasi yakwanza katika Somo la Fizikia kati ya shule 6, Geografia yakwanza kati ya shule 15, Biolojia yakwanza kati ya shule 6, Kemia yakwanza kati ya shule 6, GS ya kwanza kati ya shule 15, Hesabu ya kwanza kati ya shule 6 na Bam ya kwanza kati ya shule 9.
Kwa upande wake mmoja wa wahitimu hao, Kasimu Juma alieleza kuwa wanayomatarajio ya kufanya vizuri kuliko matokeo ya mwaka 2021 kwa sababu wamejiandaa vizuri.
Naye mmoja wa wazazi aliyekuwa na mwanafunzi anayehitimu katika shule hiyo Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Yona Katanga alimpongeza Mkuu wa wilaya hiyo kwa namna ambavyo anashirikiana na Mkuu wa shule hiyo kufanikisha matokeo bora.
Aidha, alimshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo ametoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundominu ya shule hiyo huku akiwaasa wanafunzi kutumia utandawazi kuijua dunia, kuwa wabunifu na kujua ajira zao badala ya kuutumia utandawazi kuwa wahalifu.
Wahitimu 150 ambao wanatarajia kuhitimu masomo yao toka katika shule ya Sekondari Lulumba iliyopo Wilayani Iramba mkoa wa Singida punde baada ya kuanza mitihani yao ifikapo Mei 9, 2022.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.