Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yamefanyika wilayani Iramba yakiongozwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida leo Septemba 1,2025.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “Kukuza Kisomo katika Zama za Kidigitali kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa Letu”, Mhe. Mwenda amesema kila mwanadamu ana haki ya kupata elimu, huku akisisitiza umuhimu wa elimu ya watu wazima katika kujenga jamii yenye maarifa na uwezo wa kujiajiri. “Elimu ya watu wazima ni muhimu sana katika maisha yetu kwa kupata ujuzi unaokuwezesha kujiajiri, kuondoa ujinga na kuendana na mazingira ya sasa ya kidigitali,” alisema.
Aidha, ameupongeza Mkoa wa Singida kwa mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, akibainisha kuwa kiwango cha ufaulu kimefikia asilimia 98, huku shule mpya zikijengwa ili kuhakikisha vijana wanaendelea na masomo hadi vyuo vikuu. “Sisi kama mkoa wa Singida tumejiwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya elimu na vifaa vya kujifunzia ili vijana wetu wapate fursa bora za elimu ya sayansi na teknolojia,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali, alisema elimu ndiyo msingi wa kila jambo duniani na kusisitiza shule nyingi nchini kujifunza kutoka Singida kutokana na mbinu zake za vitendo ambazo zimekuwa chachu ya mabadiliko ya jamii.
Katika taarifa yake, Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Singida Bi.Sarah Mkumbo alibainisha kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana, changamoto ya usafiri wa kufikia maeneo ya utoaji huduma za elimu bado ipo na inahitaji kupatiwa ufumbuzi.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.