DC MWENDA NA WAZIRI MWIGULU NCHEMBA WACHANGIA JUMLA YA MADAWATI 98 SHULE YA MSINGI MSANSAO ILIYOPO KATA YA MTEKENTE
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Suleiman Yusuph Mwenda amechangia madawati 28 Shule ya Msingi Msansao iliyopo kata ya Mtekente wakati wa ziara ya kamati ya Siasa Wilaya ya Iramba ilipotembelea shule hiyo Machi 10, 2025 kwa lengo la kujionea Mazingira ya utoaji wa Elimu shuleni hapo.
"Nachangia madawati 28 na nawapongeza sana kwa kuendelea kufanya vizuri katika Mtihani wa darasa la saba hongereni sana." Amesema DC Mwenda
Akiwasilisha taarifa ya shule ya Msingi Msansao kwa kamati ya Siasa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bashiri Juma Makawia Ameeleza shule hiyo ina upungufu wa madawati 88 huku ikiwa imeendelea kufanya vizuri katika taaluma ambapo kwa upande wa mtihani wa kumaliza Elimu ya msingi, asilimia ya ufaulu imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa miaka mitatu mfululizo ufaulu umepanda kutoka asilimia 25 ya mwaka 2021 hadi asilimia 74 mwaka 2024.
Kwa upande wake mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akiwakilishwa na Katibu wake Daud Madelu katika ziara hiyo amechangia jumla ya madawati 70 ili kukidhi uhitaji wa jumla ya madawati yanayohitajika kwa sasa shuleni hapo.
Katika ziara hiyo Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iramba imetoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Masimba ambayo ujenzi wake tayari umeanza na unatarajiwa kuwanufaisha Wakulima zaidi ya 24000.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamati hiyo inayongozwa na Mwenyekiti wake, Ndg. Samuel Joel Asher, wakati kamati hiyo ilipokagua na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa Wilayani Iramba.
Katika ziara hiyo, Kamati pia ilikagua miradi ya maendeleo ikiwemo Skimu ya Umwagiliaji Masimba, Ujenzi wa Nyumba ya Mwalimu (2 kwa 1) Shule ya Msingi Ushora Utemini yenye thamani ya Milioni 95 kupitia Programu ya GPE- TSP (Teachers Support Program), ambapo Hatua za Awali kwa ajili ya kuanza ujenzi zimeanza, Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Makunda kupitia Mradi wa Sequip kwa Gharama ya Milioni 544,225,626.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.