Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Mhandisi Michael Matomora amewataka wakusanya taarifa na kuweka namba za Anwani za Makazi kuwa na uvumilivu na kutekeleza jukumu hilo kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.
Matomora ametoa wito huo leo Jumanne Machi 15, 2022 wakati akifungua mafunzo ya kutekeleza zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
“Ninawaomba ndugu zanngu mkatumie maarifa yenu na kuchapa kazi kwa juhudi ya hali ya juu ili kutimiza jukumu hili la kitaifa.” Alisema Matomora
Aidha, amewataka vijana hao kutumia zoeli la Mfumo wa Anwani za Makazi kujijenga katika maisha yao na hasa wale ambao wanatarajia kupata nafasi ya kuingia katika utumishi wa umma kwa sababu wao bado ni vijana.
Kufuatia uchaguzi uliofanyika katika usaili wao, wengi waliopatikana ni vijana wenye nguvu za kutekeleza jukumu hilo la kitaifa, hivyo Mkurugenzi huyo amewataka wale ambao wanatabia ya kutumia vinywaji vyenye kulewesha kuacha katika kipindi hichi ili kutekeleza zoezi hilo kwa weledi.
Halikadhalika, amewaomba kuweka akili zao ziwe makini katika kutekeleza zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi na kuwataka kuepuka mifarakano ya aina mbalimbali.
Pia amewaonya kuwa katika kipindi cha kutekeleza zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi kuacha kuanzisha mahusiano mapya ambayo yatapelekea sintofahamu na kuharibu zoezi hili la kitaifa.
“Niwaombe ndugu zangu kwa sababu mmekubali kufanya kazi hii ni wazi mmekuwa watumishi wa umma katika kipindi hichi cha kutekeleza jukumu hili la kitaifa, hivyo mnatakiwa kuwa na nidhamu ya kiutumishi.” Alisisitiza
Akiongea katika Mafunzo hayo, Mratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi wilayani Iramba, Valerian Msigala aliwataka wakusanya taarifa na kuweka namba za Anwani za Makazi kuwa makini katika kutekeleza zoezi hilo ili serikali iweze kufikia malengo ya kuimarisha upatikanaji, utoaji na upelekaji wa huduma na bidhaa mahali stahiki.
Aidha, aliongeza kuwa kukamilika kwa zoezi hili kutarahisisha biashara mtandao, kuimarisha ulinzi na usalama, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuongeza ajira na kuimarisha shughuli za utafiti na upatikanaji wa taarifa.
Kwa upande wake mtendaji wa Kata ya Nwike wilayani hapa, Ibrahimu Kingu aliwataka wananchi kufahamu kuwa zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi litafanyika punde baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, hivyo waliunge mkono na kutoa taarifa pindi wakusanya taarifa na kuweka namba za Anwani za Makazi watakapofika katika maeneo yao.
“Natoa wito kwa wananchi wote wenye makazi katika wilaya hii kujiandaa na kulipokea zoezi hili muhimu ili kulifanikisha kwa manufaa ya Taifa letu,” Alitoa wito Kingu
Naye Bonifasi Ntui Mtendaji wa Kata ya Kidaru wilayani Iramba, alisema kuwa muitikio ni mkubwa na wananchi wanasubiri zoezi hili kwa hamu kubwa kwa sababu wamekuwa wakipata elimu ya Mfumo wa Anwani za Makazi kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.
Ntui alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kwa maono yake ya kutenga bajeti ya kutekeleza zoezi hili muhimu ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025.
“Ninaami kupitia mafunzo haya watendaji wa kata na wadau watakokwenda kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi watakuwa mabalozi wazuri katika maeneo watakayopangiwa, hivyo jamii pia itakuwa na mtazamo chanya wa kutekeleza zoezi hili.” Alisema
Zoezi za Mfumo wa Anwani za Makazi linaendelea katika wilaya na majiji nchini Tanzania.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni mwezi mmoja uliopita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipozindua oparesheni ya Mfumo wa Anwani za Makazi jijini Dodoma Februari 8, 2022.
MWISHO
Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hemedi Munga akiwaelimisha watendaji wa kata, vijiji na wakusanya taarifa na kuweka namba za Mfumo wa Anwani za Makazi manufaa ya kakamilisha zoezi hilo katika ukimbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri hiyo leo Machi 15, 2022 mjini hapa. Picha na Brian Mambuya
Watendaji wa kata, vijiji na wakusanya taarifa na kuweka namba za Mfumo wa Anwani za Makazi wakisikiliza mada za Mfumo wa Anwani za Makazi katika ukimbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri hiyo leo Machi 15, 2022 mjini hapa. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.