Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani amesikiliza na kutatua mgogoro wa Ushirika wa AWAKESHE na Muwekezaji aliyepeleka umeme katika kijiji cha Nkonkilangi kata ya Ntwike Wilayani Iramba.
Dkt Kalemani ametatua mgogoro huo leo Julai 23, 2020 wakati alipokuwa akiongea na wananchi hao katika ukumbi mdogo wa Halmashauri mjini hapa.
“Mgogoro huu ni mfupi sana kwa kuwa shughuli na rasilimali zote za kupeleka umeme kwa wananchi ni mali ya TANESCO na ndio jukumu la Serikali kupitia TANESCO kuwapelekea umeme wananchi wake,” amesema Dkt Kalemani na Kuongeza kuwa
“Serikali imekwisha toa maelekezo kuwa mwananchi yoyote hatakiwi kugharamia kifaa kimoja kimoja kama njia ya kupeleka umeme pale anapopeleka ispokuwa kulipia huduma tu na sio nguzo, waya au transifoma.”
Kwa kuwa huo ndio utaratibu wa Serikali kupitia Shirika la TANESCO kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi na sio mwanachi kugharamia vifaa hivyo.
“Ndugu wananchi! utaratibu uliotumiwa na Bwana Hussein Waziri kupeleka umeme kwa wananchi na yeye kuwa kama dalali haliwezekani na haukubaliki .” amesisitiza
Hivyo, nitowe wito kwa TANESCO kukaa ili kupiga hesabu na gharama iliotumiwa na bwana Hussein ili kumlipa fedha zake kwa kuwa mita inayotumika ni ya kwake peke yake na hivyo kuwanyima wananchi uhuru wa kuwa na mita na matumizi ya umeme na Shirika kutopata mapato ya wateja wengi.
“Ndugu zangu fahamuni kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumzuwia Mtanzania kutumia umeme anavyotaka kwa uhuru wake kwa kuwa atakuwa amezingatia taratibu na jambo hilo linainyima TANESCO kupata mapato toka kwa wateja wengi,” amefafanua Dkt Kalemani na Kuongeza kuwa
“Maana anawanyima haki wananchi ya kupata umeme moja kwa moja toka Serikalini mpaka kwa sharti lake jambo ambalo halikubaliki, pia anainyima TANESCO kupata fursa ya kuongeza wateja jambo ambalo halikubaliki kwa sababu Shirika ni lazima litafute mapato kwa kuongeza idadi ya wateja kwa uhuru wao.”
Kufuatia changamoto hiyo Dkt Kalemani ameiagiza TANESCO kumrejeshea Bwana Hussein fedha zake na mitambo kubaki kuwa mali ya TANESCO.
“Niagize Wachimbaji wanaotaka umeme kujaza fomu ili waunganishiwe umeme wao wenyewe na utaratibu wa agizo hili uanze leo mara moja ili wananchi wawe wateja wa TANESCO na sio bwa Hussein,”
“Ninaomba nipate maelezo ya meneja wa TANESCO aliye ruhusu mfumo huu Desemba mwaka jana ili tuchukue hatua na iwe marufuku kwa TANESCO Wilaya, Mkoa au Makao Makuu kumilikisha umeme kwa mtu binafsi kwa lengo la watu binafsi kuwatumia watu wengi, hatuwezi kuwa na madalali wa umeme kwa watanzania wengine,” ameagiza Dkt Kalemani
Awali akiwasilisha taarifa fupi ya namna mgogoro ulivyotokea kati ya chama cha Ushirika UWAKISHE na Mwekezaji Hussein, Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Luhahula amesema kuwa Wilaya haifurahi kuona kuwa mgogoro huu unaendelea kwa sababu unakwamisha uzalishaji.
“Kwa kweli Mhe, Waziri niliposikia unakuja nilifurahi sana maana tunajua tunapata hitimisho la mgogoro huu, ili shughuli za uzalishaji ziendelee” amesema Luhahula
Kwa upande wake mjumbe wa Ushirika wa UWAKESHE Konkilangi, Anjela Kahaya ameiomba Serikali kuwapelekea umeme katika maeneo yao ili kuwarahisishia uvutaji wa maji yanapokua yamezidi katika mashimo yanayochimbwa dhahabu.
Naye Mwakezaji wa umeme kijiji hicho, Waziri Hussein ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kusogeza nishati ya umeme katika maeneo hayo na kuahidi kuwa atashirikana na TANESCO kutekeleza agizo la Mhe, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.