IRAMBA DC YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA KIKE, WASICHANA 137 WAPEWA ELIMU KUHUSU HAKI NA ULINZI DHIDI YA UKATILI
Oktoba 13, 2025
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike katika Shule ya Sekondari Lulumba iliyopo Kata ya Old Kiomboi, ambapo jumla ya wanafunzi wa kike 137 walishiriki. Maadhimisho hayo yalilenga kuwajengea uelewa kuhusu haki, malezi na ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Wakati wa maadhimisho hayo, wanafunzi walipata mafunzo kutoka kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri akiwemo Zulfa Omary, aliyewasilisha mada kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia, na Joyce Kapinga, aliyefundisha kuhusu malezi bora na haki za mtoto wa kike.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Ndg. Mtaki Magina alisisitiza umuhimu wa kuenzi siku hii, akibainisha kuwa ni jukwaa muhimu kwa watoto wa kike kupaza sauti na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa kalenda ya Umoja wa Mataifa, tarehe 11 Oktoba kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ikiwa ni siku muhimu ya kutambua mchango na uwezo wa mabinti katika jamii. Mwaka huu maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo: "Mimi Mtoto wa Kike, Mimi Huongoza Mabadiliko: Wasichana Katika Kitovu cha Migogoro.”


KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.