IRAMBA YAHITIMISHA MASHINDANO YA UMITASHUMTA NGAZI YA WILAYA
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, imehitimisha rasmi Kambi ya Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya wilaya. Mashindano hayo yalifanyika Mei 26, 2025 katika ngazi ya Wilaya na kuanza Kambi Mei 27 hadi 29, 2025, katika Shule ya Sekondari Lulumba iliyopo Kiomboi.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu wa Awali na Msingi wa Halmashauri hiyo, Bi. Agnes Peter aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki mashindano hayo kwa nidhamu na juhudi kubwa walizoonyesha hadi kufikia hatua ya wilaya.
“Ninyi mmefika hapa kwa sababu ya nidhamu, weledi na kujituma. Tuna imani kuwa mtatuwakilisha vyema kwenye mashindano ya ngazi ya mkoa na hata Taifa. Endeleeni kupambana kwa bidii ili kurudi na ushindi nyumbani,” alisisitiza Bi. Agnes wakati wa hafla ya kufunga kambi hiyo tarehe 28 Mei, 2025.
Kwa upande wake, Afisa maendeleo ya michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Ndugu John Mghana, alieleza kuwa mashindano hayo yamelenga kubaini, kuibua, kuendeleza na kuvitangaza vipaji vya michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi. Alibainisha kuwa ushindani kutoka kwa wanafunzi wa kata mbalimbali umechangia kwa kiasi kikubwa kupata wachezaji bora watakaoiwakilisha Iramba katika ngazi ya mkoa.
Mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa wa Singida yanatarajiwa kuanza rasmi Mei 30, 2025, yakibeba kaulimbiu isemayo: “VIONGOZI BORA NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAALUMA, SANAA NA MICHEZO. SHIRIKI UCHAGUZI MKUU 2025 KWA AMANI NA UTULIVU." na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 6, 2025.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.