IRAMBA YANUFAIKA NA HUDUMA YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS DKT. SAMIA
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ni miongoni mwa Halmashauri saba za Mkoa wa Singida zilizopokea huduma ya Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, waliotoa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi kuanzia Oktoba 6 hadi 10, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Oktoba 10, 2025 hospitalini hapo, Afisa Tawala Bi. Dorothy Mwangamila alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hiyo, sambamba na kuwashukuru madaktari bingwa kwa kujitoa kutoa huduma hizo muhimu karibu na wananchi.
“Nianze kwa kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa programu hii. Nawashukuru pia kwa kujitoa kwenu kuja katika hospitali hii kutoa huduma hizi za kibingwa… Huduma hizi zimekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba,” alisema Bi. Mwangamila.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dkt. James Komanya, alisema kuwa mwezi Oktoba 2025 jumla ya wagonjwa 345 walipata matibabu kupitia programu hiyo ya Madaktari Bingwa, ikilinganishwa na wagonjwa 425 waliopatiwa huduma mwezi Mei mwaka huu.
Alibainisha kuwa kupungua kwa idadi hiyo kunatokana na huduma hizo kufanyika mara kwa mara wilayani Iramba, jambo linalowasaidia wananchi wengi kupata matibabu mapema na kwa urahisi zaidi.
Huduma hizo ni sehemu ya Programu Maalum ya Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayotekelezwa katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza gharama za kusafiri kufuata huduma hizo mbali.



KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.