IRAMBA YAWAAGA WAHESHIMIWA MADIWANI KWA HESHIMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Ndugu Michael Agustino Matomora, amewapongeza Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri hiyo katika hafla maalum ya kuwaaga rasmi baada ya kumaliza kipindi chao cha uongozi wa miaka mitano tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Tukio hilo lilifanyika tarehe 18 Juni 2025, katika viwanja vya ofisi ya Halmashauri, na kuhudhuriwa na viongozi wa Dini, Serikali, pamoja na watumishi wa umma kutoka ofisi ya makao makuu ya wilaya hiyo.
Katika hotuba yake ya shukrani, Mkurugenzi Matomora ametoa Pongezi za dhati kwa Waheshimiwa Madiwani kwa kuonesha mshikamano na uzalendo katika kipindi chao cha uongozi.
“Ninatoa pongezi kwa Waheshimiwa Madiwani kwa kushirikiana nasi katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Mmeonesha uongozi bora na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi,” alisema Mkurugenzi Matomora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mhe. Innocent Msengi ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kyengege amewashukuru wa wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wataalam wengine wa Halmashauri kwa ushirikiano hasa katika Usimamizi wa miradi ya maendeleo wilayani Iramba. Pia amewashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa ushirikiano wakati wote wa Uongozi wao katika Halmashauri hiyo.
Hafla hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda, iliambatana na utoaji wa vyeti vya pongezi kutambua mchango wa madiwani hao, ikiwa ni ishara ya heshima na shukrani kwa juhudi zao katika maendeleo ya Halmashauri.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.