Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Bw. Suleiman Yusuph Mwenda, ameitaka jamii kutokufumbia macho vitendo vyote vinavyohatarisha au kuchangia uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Mwenda ameyasema hayo Jumatano, Disemba 3, 2025, wakati wa mkutano wake na wazee maarufu, viongozi wa dini,viongozi wa vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na wenyeviti wa vitongoji kutoka Kata za Kiomboi na Old Kiomboi.
"Ndugu zangu, ninyi ni viongozi na mna dhamana kubwa sana. Tuendelee kuhubiri amani kwa watu tunaowaongoza, kwani amani ndiyo msingi wa maendeleo katika nchi yetu," alisema DC Mwenda.
Aidha, amewataka viongozi wa maeneo hayo kuendelea kutoa taarifa mapema pindi wanapomtilia shaka mtu yeyote mgeni anayeingia kwenye mazingira yao bila kujulikana, ili kuimarisha ulinzi na kuzuia matukio yanayoweza kuhatarisha usalama.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa kitongoji cha Zahanati Bwana Ramadhani Masanja ameiomba serikali ya wilaya kuendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa vijiji na vitongoji ili kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inabaki kuwa ya kuridhisha.
"Mheshimiwa DC, hali ya ulinzi katika maeneo yetu iko vizuri, na tunaendelea kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha tunadumisha usalama kila wakati," alisema Masanja.

KIOMBOI, IRAMBA
Postal Address: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Telephone: 026 - 2532253
Mobile: 026 - 2533001
Email: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.