Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wilayani Iramba, Suleiman Mwenda amesema kuwa falsafa, maono, maarifa na imani ya Rais Samia kujenga madarasa nchini imeleta tija ya wanafunzi kuanza masomo yao bila ya kikwazo chochote.
Mwenda ameyasema hayo mwishoni mwa juma hili wakati akiwa na Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida wilayani Iramba katika shule ya sekondari Kinambeu mjini hapa.
Ziara hiyo inajiri ikiwa ni siku chache tangu wanafunzi wafungue shule kute nchini.
Alisema kuwa wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za ujenzi wa madarasa ambayo yamekidhi mahitaji ya wanafunzi wote.
“Ndugu Mwenyekiti, tumshukuru Rais Samia kwa namna ya kipekee kwa fedha alizoleta, tumeweza kujenga madarasa 47 na kuweza kukidhi wanafunzi 1250.” Alisema
Aidha, aliongeza kuwa wanafunzi ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ni wanafunzi 4022 ambapo ni ongezeko la takribani wanafunzi 800 ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliochaguliwa mwaka jana.
Alibainisha kuwa kama madarasa haya yasingejengwa kungekuwa na wanafunzi 1200 ambao wasingekuwa na madarasa ya kusomea lakini kwa ujenzi wa madarasa haya wanafunzi wote wanapata sehemu ya kusomea na ziada ya takribani wanafunzi 80.
“Kwa kweli tunamshukuru Rais Samia kwa sababu tumepata madarasa ambayo yanasamani zote ikiwemo meza, viti pamoja na ofisi za walimu.”
Halikadhalika, Mwenda amekipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa na ilani nzuri ambayo inaielekeza serikali kwamba wanafunzi wote wanaochaguliwa kujiunga na masomo kwa mwaka husika lazima wapate sehemu za kusomea na kuwa na mazingira bora.
Akiongea katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo umeboresha manzari ya shule na mji kwa ujumla.
“Hii ndio manzari ya kiomboi, leo unapoingia wilayani unakuta shule imependeza namna hii, hakika hili ni jambo la faraja sana.” Alipongeza
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Michael Matomora kuona namna ya kuhakikisha shule ya Sekondari Kinambeu inapata bwalo la wanafunzi.
Awali akiwasilisha taarifa fupi mbele ya Kamati hiyo, Mkuu wa shule ya Sekondari Kinambeu, Godfrey Yohana amemuhakikishia Mwenyekiti huyo, kuwa watayatumia madarasa hayo kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanafaulu vizuri.
Kw upande wake mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo ambaye yupo kidato cha kwanza, Warda Mohammed amemshukuru Rais Samia kwa kusaidia kuwaletea fedha za ujenzi wa madarasa na madawati ambayo itakuwa rahisi kwao kusoma, kuandika na kuokoa muda.
Aidha, ameongeza kuwa madawati hayo yamepunguza mzigo uliokuwepo wa kuwataka wazazi kupeleka madawati shuleni.
Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilitembelea mradi wa maji kata ya Maluga, mradi wa shule shikizi kata ya Ulemo na Mradi wa madarasa kata ya Old Kiomboi wilayani Iramba.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.