KAMATI YA FEDHA, UONGOZI NA MIPANGO YA HALMASHAURI YA WILAYA YA IRAMBA YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025, kwa lengo la kufuatilia utekelezaji na thamani ya fedha kwenye miradi hiyo.
Ziara hiyo ilifanyika, 24 Aprili 2025 ambapo kamati ilitembelea miradi kadhaa inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya, ikiwemo: Mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Yombo wenye thamani ya shilingi milioni 318.8, Ujenzi wa Shule ya Msingi Nkokilangi (Mil. 250), Ujenzi wa Zahanati ya Mseko (Mil. 250), Ujenzi wa Shule mpya ya Amali katika Kijiji cha Kitukutu (Bil. 1.6), Kituo cha Kilimo cha Mampanta (Mil. 109.72).
Akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi, alieleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Msingi Yombo, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya ujenzi kwenye miradi mingine hususan Shule mpya ya Amali Kitukutu pamoja na Zahanati ya Mseko.
Aidha, Msengi alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo. Pia alitoa Pongezi kwa Mbunge wa Iramba Magharibi na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na viongozi wengine kwa juhudi zao za kuwahudumia wananchi wa Iramba.
“Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za miradi hii. Pia nampongeza Mbunge wa Iramba Magharibi na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuwahudumia Wananchi wa Iramba, Pongezi pia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa usimamizi mzuri. Rai yangu ni kwamba usimamizi uendelee ili miradi ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaostahili,” alisema Mheshimiwa Msengi.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.