Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni amegawa ndoo za maji ya kutiririka 282 na sabuni katoni 12 kwa Wazazi wa Watoto wanaohudumiwa na Kanisa la EAGT Kiomboi wakishirikiana na Compassion International Tanzania.
Mwageni amegawa vifaa hivyo leo May 24, 2020 baada ya ibada fupi iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la EAGT mjini Kiomboi.
Amewaagiza wazazi wote waliopatiwa vifaa hivyo kuvitumia ili kuendelea kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona na sio kwenda kuviweka kama mapambo katika majumba yao.
Pia, amewaomba kuacha tabia ya kuwatumia wanafunzi katika shughuli za uchumi kama vile kuwapeleka sokoni, madukani na minadani ili kuwaepusha na maambukizi ya corona.
“Niwaombe wazazi wenzangu kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha 6 na vyuo kwa kuwanunulia barakoa, sanitaiza na pesa kwa ajili ya kununua machungwa, malimao na Tangawizi,” ameomba Mwageni na kuongeza
“Kwa upande wa kidato cha pili na cha nne Halmashauri imeandaa Makala mbalimbali ambazo zitawafikia wanafunzi hao kupitia watendaji wa vitongoji vyao.”
Halikadhalika, Mwageni amewaagiza Wazazi hao kuwahimiza wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha kwanza, tatu, na cha tano kutumia muda wao kutazama vipindi vya masomo mbalimbali vinavyorushwa na Chanel Ten, Azam TV, TBC na ZBC.
“Katika kipindi hichi cha kusubiria maelekezo ya Serikali ,wanafunzi wanawajibu wa kubadilisha namna ya kujifunza kutoka darasani hadi barazani kwa kutazama vipindi vya masomo mbalimbali kupitia Chanel Ten, Azam TV, TBC na ZBC,” amesema Mwageni
Katika hatua nyingine, Mwageni amemshukuru Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Robert Kijanga kwa kuwalea watoto hao, kwani kitendo hicho kimeifanya Wilaya ya Iramba kutokua na Watoto wa mitaani na omba omba.
Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT kiomboi, Robert Kijanga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna alivyopambana na janga la corona bila kufunga Makanisa, Misikiti na shughuli za kiuchumi.
“Rais huyu ameishangaza Dunia nzima kwa namna alivyopambana na janga la corona kwa kuweka rehani maisha yake kwa Mungu kuliko kujifungia ndani bila Mungu, ameruhusu Makanisa na Misikiti waumini waendelee kumuomba Mungu, na ndio maana tunakabiliana na corona vyema na kwa sababu hiyo leo tumeshinda na leo ni siku ya pekee na ya kumshukuru Mungu kwa kuwa tumeshinda,” amesema Kijanga na kuongeza
“Mhe, Rais ameliokoa Taifa kuto kuingia katika hali mbaya kwa kuwa tumeendelea kuchapa kazi, leo hii Mataifa Makubwa yalioendelea yalijifungia na leo yanajifungua na kutukuta pale pale tulipokuwepo.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Huduma ya Mtoto wa Kanisa la EAGT, Gerald Adoltia alipokua akitoa taarifa fupi mbele ya Mkurugenzi Mtendaji, Linno Mwageni amesema kuwa wamekuwa na utaratibu wakutoa elimu ya kiroho, kimwili, kiuchumi na kijamii kila siku ya jumamosi kwa watoto 282 tangu Novemba 14, 2014.
Akibainisha malengo ya kuwafundisha watoto hao kujikomboa toka katika umasikini, amesema kuwa wamekua wakiwapatia watoto hao daftari, viatu, nguo za shule, kalamu, mabegi na kugharamia matibabu pindi wanapougua.
Pia, kutoa mitaji kwa familia takriban 75 ambapo jumla ya Tshs 10milioni zimetumika kuzinufaisha familia kuboresha maisha yao kiuchumi bila kudai fidia wala marejesho yoyote kutoka kwao.
Familia hizo zimekuwa zikipatiwa mafunzo ya Afya, ujasiriamali wa nadharia na vitendo, ufugaji, malezi ya familia na ndoa, kilimo, ulinzi wa mtoto, elimu ya fedha na mipango pamoja nakujengewa uwezo wa kupambana na magonjwa ya ukimwi na malaria.
Naye mmoja wa Wazazi waliogawiwa vifaa hivyo, Martha Edson amewashukuru viongozi wa Kanisa la EAGT kwa kuwapatia ndoo na sabuni na kuwaombea Mungu awabariki.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akiwaasa wazazi kuwanunulia wanafunzi barakoa na kuhakikisha wanawahimiza Wanafunzi kufuatilia vipindi vya masomo kwenye Chaneli Ten, TBC, ZBC na Azam TV. Picha na Hemedi Munga
Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiomboi akiombea Wilaya ya Iramba na Taifa kuepukana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. Picha na Hemedi Munga
Mdhibiti wa maambukizi ya corona wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Yona Mwasanga akiwaonesha Waumini wa Kanisa la EAGT namna ya kunawa na kusugua viganja vya mikono kwa vitendo ili waendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akiwa na Mchungaji Robert Kijanga pamoja na wataalam wengine punde baada ya kugawa ndoo na sabuni. Picha na Hemedi Munga
Ndoo 282 na katoni 12 za sabuni zilizotolewa na Kanisa la EAGT Kiomboi kwa Wazazi wa Watoto wanaohudumiwa na Kanisa hilo kwa kushirikiana na Compassion International Tanzania. Picha na Hemedi Munga
Ndoo 282 na katoni 12 za sabuni zilizotolewa na Kanisa la EAGT Kiomboi kwa Wazazi wa Watoto wanaohudumiwa na Kanisa hilo kwa kushirikiana na Compassion International Tanzania. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.