Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi amefungua mafunzo ya siku moja ya mfumo wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao (TANePS) kwa Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu wakuu wa shule za Msingi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Alhamisi Januari 16, 2020 katika Ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mjini Kiomboi.
Dkt, Lutambi amewaagiza viongozi hao kutimiza wajibu wao na kuhakikisha kuwa kila kitu katika taasisi zao kinafuata sheria, taratibu na kanuni na miongozo kama ilivyoagizwa na Serikali.
‘’Serikali ya sasa imeamua kupeleka pesa katika mamlaka zenu kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na hivyo sheria haitambui endapo kiongozi au mtumishi aliyoko chini ya kiongozi huyo atakapoharibu,
mmekabidhiwa dhamana ya kuhakikisha pesa zinazoletwa na serikali zinatumika katika malengo stahiki.”
“ Nyinyi ni maafisa masuuli na mnao wajibu kuhakikisha taratibu zote za manunuzi zinazingatiwa,” amesisitiza Dkt, Lutambi
Kufuata taratibu na kanuni za manunuzi zitapunguza uwepo wa hoja za ukaguzi zitokanazo na manunuzi wilayani hapa.
Aidha Dkt, Lutambi amewataka viongozi hao kutumia mfumo wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao (TANePS) ambapo mwisho wa kufanya manunuzi nje ya mfumo ilikuwa Desemba 31mwaka jana.
Hatua hiyo itasaidia serikali kufahamu manunuzi yanayofanyika katika kila mwezi na hivyo kuiwezesha kupanga mipango yake.
Hata hivyo amewatahadharisha viongozi hao watakaofanya manunuzi nje ya mfumo wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao na kukwamisha shughuli mbalimbali katika taasisi husika hawatoeleweka.
Amefafanua kuwa mfumo huo unaleta uwazi unaomuwezesha msambazaji yoyote wa bidhaa aliyesajiliwa kuwa anaweza kusambaza bidhaa hata kama atakuwa mkoa mwingine.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni amewakumbusha viongozi hao kuwa pamoja na kuwa swala la manunuzi sio fani walizosomea bali wanapaswa kufahamu kuwa barua walizopewa na mwajiri wao zinawataka kutekeleza na majukumu mengine watakayopangiwa.
Awali akielezea mzunguko wa manunuzi Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Afisa manunuzi na Ugavi , Ibrahimu Nkumbi amesema manunuzi ni hatua kwa hatua zinazojumuisha shughuli muhimu zinazohitajika katika kukamilisha manunuzi.
Nkumbi amezitaja hatua hizo kuwa ni utambuzi wa mahitaji ya manunuzi, kupanga mpango wa manunuzi, mchakato wa manunuzi, utoaji tuzo ya mkataba, utekelezaji usimamizi wa mkataba na tathimini ya mkataba.
Akichangia mada mkuu wa shule ya Tumaini Sekondari, Honoratha Mbiaji amemuhakikishia Katibu Tawala huyo kuwa mafunzo hayo wanayoyapata watayafanyia kazi kwa ukamilifu.
Naye Mkuu wa Shule ya Lulumba Sekondari, Jeremia Kitiku ameuomba uongozi kufikisha mafunzo hayo kwa sekta mbalimbali ikiwemo afya.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Afisa manunuzi na Ugavi , Ibrahimu Nkumbi akiwafafanuliya Wakuu wa Shule mzunguko wa manunuzi katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Iramba. Picha na Hemedi Munga
Wakuu wa Shule (TAHOSA) na Walimu wakuu (TAPSHA) wakifuatilia mafuzo kwa umakini katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba. Picha Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.