Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Songoma ameihamasisha jamii kuzingatia usawa wa kijinsia unaompa Mwanamke usawa na Mwanaume katika masuala ya elimu, uongozi na fursa za kiuchumi ili wawe chachu ya kuleta maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Songoma amehamasisha usawa huo leo Jumapili Machi 8, 2020 wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliofanyika katika kijiji cha Doromoni kata ya Tulya Wilayani Iramba.
Ameiasa jamii kuacha dhana potofu kuwa Wanawake ni viumbe zaifu ambao hawawezi kuleta Maendeleo katika jamii zaidi ya kupika, kuzaa watoto na kuwalea.
Kufuatia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “ Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadae,” Songoma amesema kuwa suala la usawa linapaswa lianzie ngazi ya familia na jamii kwa ujumla kwa kuwapa nafasi watu wa jinsia zote katika masuala ya mirathi, umiliki wa rasilimali, uwongozi na elimu.
“Ndugu wananchi tambueni kuwa serikali inawathamini wanawake kwa kuchukuwa juhudi ya kupigania maslahi ya Wanawake kwa kuweka mikakati ya utekelezaji na usimamizi wa sera na sheria mbalimbali zinazomlinda Mwanamke,” amesisitiza Songoma
Aidha amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imehakikisha usawa wa kijinsia kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za binaadamu hasa Wanawake huku akionesha takwimu za watoto wa kike wanaoendelezwa kielimu kuongezeka.
Pia Halmashauri kwa kushirikiana na Mashirika yasiokuwa ya kiserikali imekuwa ikiwahamasisha Wanawake kujiunga kwenye vikundi vya kiuchumi, vikundi vya kifedha vya kijamii na kujengewa uwezo kuhusu stadi mbalimbali za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kupatiwa mikopo inayotolewa kutoka katika 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Halmashuri kupitia mapato ya ndani imetumia takribani Tshs64.35 milioni kukopesha vikundi 30 vya kiuchumi ambapo vijana walikuwa vikundi 11, wanawake vikundi 13 na vikundi vya watu wenye ulemavu 6.
Halikadhalika kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana unaotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana , Ajira na Watu wenye Ulemavu Halmashauri imetumia Tshs37 milioni kukopesha vikundi 9 vya vijana wa kiume na kike.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi wa kilele cha maadhimisho hayo,Betha Edward mkazi wa Kizega ameiomba jamii kulinda, kuheshimu na kahakikisha haki za wanawake kiuchumi, kijamii na kiutamaduni zinapatika.
Nao Wakina mama wa kwaya ya Doromoni wameiomba jamii kutambua kuwa wakinamama ni jeshi kubwa linalopaswa kuheshimiwa na kutambua kuwa Wanawake ni nguzo ya jamii na Taifa.
Pia wameitaka jamii kupiga vita migogoro, mimba za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia, udini, ukatili na tofauti za kirangi zidi ya mwanamke.
Naye katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Iramba, Ibrahim Mjanaheri amewataka Wanawake kuacha tabia ya kusema wakiwezeshwa wanaweza.
Mjanaheri amewaambia Wanawake hao kuwa wao wanaweza kwa kuwa tayari walikwisha weza kumuweka mwanaume katika matumbo yao.
“ Wanawake ndio nguzo ya familia kuna nani mwingine anaweza kuiwezesha nguzo baada ya kuwepo, maana yake ni kwamba nguzo yenyewe inaweza kujiwezesha,” amesisitiza Mjanaheri
Chimbuko la siku ya Wanawake Duniani lilitokana na mkutano wa kimataifa uliofanyika Beijing China mwaka 1975 wakijadili haki za kibinaadamu za unyanyasaji, ubaguzi wa kijinsia na kuhakikisha wanawake wanahusishwa katika shughuli za kimaendeleo.
Kufuatia azimio la mkutano huo waliridhia kuwa kila mwaka machi 8 kuadhimisha kwa kuangalia mafanikio na changamoto zinazowakabili Wanawake katika ushiriki wa maamuzi kwa shughuli za maendeleo.
Nayo serikali ya Tanzania kutokana na azimio hilo mwaka 1992 ilipitisha sera ya maendeleo ya Wanawake na kuanza kuitekeleza.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akiwataka Wanawake kujiunga kwenye vikundi ili wapate mikopo inayotokana na 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo. Picha na Hemedi Munga
Katibu wa Chama cha Mapinduzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Ibrahim Mjanaheri akiwafunda Wanawake kuwa wao ni nguzo ya familia na jamii inayoweza kusimama yenyewe bila kuwezeshwa. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Jane Ng’ondi akisoma vikundi mbalimbali vilivyonufaika kwa kupewa mikopo inayotokana na 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo. Picha na Hemedi
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Songoma akionesha kadi ya iCHF iliyoboreshwa ambayo kikundi cha peace and love kimewakatia watoto wenye mahitaji maalum, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Iramba, Samwel Joel na kulia mwa Katibu huyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni. Picha na Hemedi Munga
Kikundi cha peace and love cha mjini kiomboi kikitoa ushuhuda wa namna walivyoweza kuwakatia kadi ya iCHF iliyoboreshwa watoto wenye mahitaji maalum wa shule ya msingi Kizega kutokana na michango yao iliyoanzia na mtaji wa milioni mbili hadi kufikia 30 milion. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa pili kutoka upande wa kushoto akiwa na baadhi ya Wakuu wa Idara wakifuatilia kwa kina kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliofanyika katika kijiji cha Doromoni kata ya Tulya Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya akina mama na watoto wakiwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliofanyika katika kijiji cha Doromoni kata ya Tulya Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Umati wa akina mama na watoto wakiwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliofanyika katika kijiji cha Doromoni kata ya Tulya Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Umati wa akina mama na watoto wakiwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliofanyika katika kijiji cha Doromoni kata ya Tulya Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.