Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi emegawa kompyuta kwa shule za Halmashauri ya Wilaya ya Iramba zilizoingia kumi bora kimkoa Singida matokeyo ya mwaka 2019.
Lutambi amegawa kompyuta hizo (desktop) mwishoni mwa juma hili wakati alipokua akiongea na Baraza maalum la Madiwani kujibu maagizo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mjini Kiomboi.
Ametumia nafasi hiyo kumshukuru aliyetoa kompyuta hizo hasa katika nyakati hizi ambazo kila kitu kinaendeshwa kielektroniki.
“Kwa sasa ni zama za kielektroniki, nilazima tushukuru kwa kupata kompyuta hizi kwa sababu walimu watatekeleza majukumu ya kielimu, Serikali na kuandaa mitihani na majaribio mbalimbali ya wanafunzi ili waweze kufanya vizuri,” amesema Lutambi nakuongeza
“Kompyuta hizo zitawasaidia walimu kupata maarifa mapya na marejeo mbalimbali ili kujipatia maarifa mapya kulingana na masomo yao wanayofundisha, hivyo kuwa na weledi na kupata mawazo mapya yanayoendana na wakati huu tulionao.”
Hatua hiyo itawasaidia Walimu kuondokana na matumizi ya notsi za zamani walizozitumia wao wakiwa shuleni, huku akiwasihi kuzitumia vizuri.
“Niwasihi ndugu zangu Wakuu wa Shule kuwa kompyuta hizi sio binafsi, zimetolewa kwa shule na nyinyi mmekuja zipokea kwa niaba ya shule zenu, kwa hiyo niwaombe kwa kushirikiana na walimu wenzenu mkazitumie vizuri,” amesisitiza Lutambi
Kompyuta hizo zilizogawiwa kwa shule hizo ni ahadi ambayo aliahidi Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba alipokua akizungumza katika Baraza la Madiwani Juni 02 mwaka huu.
“Ninawapatia kompyuta mpya za kisasa za shule nne zilizoingia kumi bora kimkoa Singida ili kuweza kusaidia taratibu hizi za kisasa za uandaaji wa masomo ya wanafunzi,” alisema Waziri Nchemba
Lengo likiwa ni kuwachochea Walimu kwa kazi nzuri wanazo zifanya chini ya usimamizi mzuri wa Mkuu wa Wilaya yetu, Emmanuel Luhahula.
Akishuhudia ugawaji wa kompyuta hizo kwa shule zilizokua na ufaulu mzuri matokeo ya mwaka jana, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo, Godfrey Mwanjala amesema kuwa kompyuta hizo zitasaidia maandalizi mbalimbali ya majukumu ya walimu kwa wanafunzi wao.
Mwanjala amezitaja shule hizo kuwa ni Kyengege Sekondari, Kisana Sekondari, Mgongo Sekondari na Kidaru ambazo zimeingia kumi bora kimkoa Singida.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Shule waliopatiwa kompyuta hizo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mgongo, Lameck Ayieko ameshukuru kwa kupatiwa msaada huo wa kompyuta na kuahidi kuwa watazitumia kwa manufaa ya shule zao na kuzituza vizuri.
MWISHO
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mgongo, Lameck Ayieko akipokea kompyuta toka kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba zilizogawiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati wa kikao maalum cha kushughulikia maagizo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Picha na Hemedi Munga
Afisa Elimu kata ya Kyengege, Daudi Kachilu akipokea kompyuta kwa niaba ya Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kyengege zilizotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba zilizogawiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati wa kikao maalum cha kushughulikia maagizo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Baadhi ya Kompyuta zilizotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba zilizogawiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati wa kikao maalum cha kushughulikia maagizo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.