Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Nchini Godrey Mnzava, ameziagiza Halmashauri nchini kutenga fedha za kukabiliana na ugonjwa wa malaria kama agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan linavyotaka.
Mnzava ametoa agizo hilo Wilayani Iramba mkoani Singida wakati anakagua afua za lishe na kuonyesha kutorishishwa na kasi ya baadhi ya Halmashauri katika kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa Malaria.
Mnzava amesistiza kuwa agizo la Rais Samia ni lazima litekelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huo wa Malaria uwe umetokomezwa kabisa hapa nchini.
"Tengeni bajeti kwa kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria kwa sababu bado unaathiri nguvu kazi ya Taifa," amesisitiza Mnzava.
Ametoa mfano kwa Halmashauri ya Iramba ambayo inakusanya zaidi ya bilioni Mbili kwa mwaka kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato lakini imeshindwa kutenga shilingi milioni Saba kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria jambo ambalo amesema sio zuri na halifurahishi hata kidogo.
Kuhusu matumizi ya dawa za kulevya, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuimarisha misako ambayo itasaidia kuwakamata watumiaji na wafanyabiashara za dawa hizo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema tatizo hilo lisipokomeshwa litaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo ni muhimu kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya uzambaji na utumiaji wa dawa za kulevya ikiwemo kuwabaini watu kwa siri watu wanaofanya biashara ili waweze kukamatwa na kuwajibishwa.
Baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Iramba wamemwahidi Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kuwa watatekeleza maagizo yake aliyoyatoa kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa wilaya ya Iramba na mkoa wa Singida kwa ujumla.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.