Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Shule ya Sekondari Lulumba,Jeremia Kitiku amesema kuwa Lulumba Sekondari imekuwa ya kwanza Kimkoa kati ya shule 12 za Mkoa wa Singida na ya 23 Kitaifa kati ya shule 586 katika matokeo ya Kidato cha Sita yaliotangazwa na Katibu wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt, charles Msonde.
Kitiku ameyasema hayo leo ijumaa agosti 21, 2020 wakati akiongea na mwandishi wetu katika viwanja vya Shule hiyo mjini Kiomboi.
“Nijambo la Kumshukuru Mungu na kuwapongeza Wanafunzi kwa matokeo mazuri waliyoyapata yanafurahisha sana,” amesema Kitiku na kufafanua kuwa
“Wanafunzi waliofanya Mtihani walikuwa 151 ambapo 85 wamepata daraja la kwanza, 53 daraja la pili, 13 daraja la tatu na hakuna aliyepata 0,”
Kufuatia hatua hiyo amewapongeza Walimu wa Shule kiyo ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi unaongezeka ili kuifikisha Shule hiyo ndani ya kumi bora kitaifa.
“Ndugu walimu wenzangu nawapongeza sana kwa kazi na juhudi kubwa mnazozifanya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa vizuri kabla ya mtihani wa Taifa, hivyo leo tunasherehekea matokeo mazuri” amepongeza na kuongeza kuwa
“Kwa masomo ya jografia, fizikia, kemia, baiolojia, hesabu, GS na bam yanayofundishwa hapa tumeshika nafasi ya kwanza kimkoa na kushika nafasi nzuri kitaifa”
Akieleza siri ya mafanikio hayo Mkuu huyo wa Shule, amesema kuwa huwa wanatekeleza mkakati wa kumaliza silabasi mapema kisha wanafanya marudio na kuwatahini Wanafunzi Mitihani ya mara kwa mara.
Amebainisha kuwa wanao ushirikiano wa kimasomo na mitihani na shule ambazo zinafanya vizuri Kitaifa ikiwemo Tabora boys.
Akizungumzia ari na kasi ya walimu wanaojitoa kutekeleza mikakati hiyo amesema kuwa ni zawadi mbalimbali zinazotolewa na Shule ikiwemo Tsh 20,000 pindi Mwalimu anapofanikisha Mwanafunzi kupata A, na Tsh 10,000 mwanafunzi anapopata B, Hivyo kuongeza ari ya kujituma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Tunahakikisha kuwa Walimu wanapata chai na kitafunwa asubuhi chakula cha mchana kwa Walimu wote kwa gharama za Shule hivyo kuwafanya walimu kufundisha kwa ushindani,” amebainisha
Akibainisha mbinu na njia anazozitumia Mwalimu wa Jografia aliyefanikisha somo hilo kushika nafasi ya sita kitaifa, Daud Noa amesema kuwa ni mara ya kwanza kwa somo hilo kufundishwa katika shule hiyo kwa sababu mchepuo huo haukuwepo.
“Ni mara ya kwanza kwa mchepuo unaohusisha somo la jografia katika shule yetu, hivyo tumefanikiwa kushika nafasi ya sita kati ya Shule 737 kitaifa huku kimkoa na kiwilaya kushika nafasi ya kwanza,” amesema Noa
Mikakati iliyotumika ilikua mingi ikiwemo kumaliza silabasi mapema na kufanya marudio ya mada mbalimbali pamoja na kuzifanyia mitahani ya ndani na nje.
Kwa upande waka kiranja wa Taaluma wa Shule hiyo, Gratnes Mlashan amesema kuwa matokeo ya Kidato cha Sita wameyapokea vizuri kwa sababu yamewafurahisha na kuwatia moyo kuendelea kufanya vizuri mitihani inayokuja.
“Natoa wito kwa wanafunzi wenzangu kusoma kwa bidii kuhakikisha kuwa matokeo haya hatushuki ispokuwa tupate matokeo zaidi ya haya,” amesisitiza Mlashan
Naye Kiranja Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi katika Shule hiyo, Ernest Munishi amesema kuwa matokeo ya Kidato cha sita yamekuwa ni msingi mkubwa kwao kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kuzingatia maelekezo ya walimu wao ili wafaulu zaidi.
“Ndugu zangu wanafunzi fahamuni kuwa kila kitu kinawezekana kama walivyoweza kufaulu wenzetu, sisi tufaulu zaidi na kuingia kumi bora inawezekana,” ametilia mkazo Munishi
Ufaulu wa Shule ya Sekondari Lulumba umeongezeka kwa Mwaka wa masomo 2020 ukilinganisha na mwaka 2019 ambapo ilishika nafasi ya pili kimkoa na ya kwanza kushikwa na Shule ya Sekondari Mwanamwema
MWISHO
Mkuu wa Shule ya Lulumba Sekondari, Jeremia Kitiku akielezea mikakati iliyowawezesha wanafunzi 151 kufaulu na kuwa yakwanza Mkoa wa Singida ya 23 Kitaifa. Picha na Hemedi Munga
Mwalimu wa Jografia Shule ya Lulumba Sekondari, Daud Noa akielezea mikakati aliyotumia kuifanya Shule hiyo kushika nafasi ya sita kwa Somo la Jografia Kitaifa kati ya Shule 737 na ya kwanza kimkoa. Picha na Hemedi Munga
Kiranja wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Lulumba, Gratnes Mlashan akihadi kuwa wanahitaji kuingia kumi bora kitaifa matokeo ya mitihani itakayofuata. Picha na Hemedi Munga
Kiranja Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi, Ernest Munishi akieleza namna matokeo ya kidato cha sita yalivyoamsha ari ya kujisomea na kufuata maelekezo ya walimu wao ili waweze kufaulu zaidi. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.