Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Samwel Shillah amekipa siku 90 kikosi kazi cha Corparation Sole Surperitandents kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya Shelui.
Shillah ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki hii alipotembelea Kata ya Shelui akiwa na kamati ya Fedha, Mipango na Utawala wa Halmashuri ya Wilaya ya Iramba.
“Fedha tunazo, hivyo tunawaomba wenzetu wa kikosi kazi kumaliza kazi hii kwa wakati kwani hakuna kikwazo chochote,” ameagiza Shillah na kuongeza
“Tunataka baada ya muda mchache wananchi waone matokeo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Shelui na kupata huduma za Afya.”
Shillah amefafanua kuwa Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akishatoa fedha anataka aone matokeo kwa haraka.
“Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akisha toa pesa, msifikirie kua hayupo hapa, ulipo tupo” amesisitiza Shillah
Halikadhalika, amewataka Wataalamu kuhakikisha wanafika eneo la mradi wa kituo cha Afya Shelui kuona mwenendo wa kazi kila siku.
Pia, amemtahadharisha Mganga Mkuu wa Zahanati ya Shelui, Alex Mpweku kuwa makini na mtulivu katika mradi huu.
“Asilimia 90% Mganga wa Zahanati ya Shelui ujenzi huu upo chini yako, hakikisha unapoandika kitu au kupitisha pesa yoyote umesoma kuanzia neno la kwanza hadi la mwisho na unapoona kua umechoka usifanye kazi hii,” amesisitiza Shillah na kuongeza
“Ninakuomba uwe mtulivu katika mradi huu, ili mwisho wa siku uweze kufika mbali maana mradi huu unaweza kukupandisha au kukushusha cheo.”
Amemtaka Mganga huyo kufaham kuwa changamoto zitakua nyingi pamoja na maelekezo mbalimbali kutoka kwa viongozi mbalimbali.
“Angalia mliyokubaliana, tembea kwenye mstari, mtu akitaka kubadilisha neno mwambie alete kwa maandishi ili kesho na keshokutwa unatoa nyaraka, lakini mimi nikija na kukwambia vunja hapa na ukavunja, fahamu kuwa gerezani utakwenda peke yako maana kazi za serikali zinafanyika kwa maandishi,” amesisitiza Shillah
Katika hatua nyingine,Makamu Mwenyekiti huyo amewataka Wanakamati wa ujenzi wa kituo cha Afya Shelui kuenedelea kushirikiana katika ujezi huo ili uende kwa haraka nakufanikisha kukamilisha kituo hicho ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi.
Mapema akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Shelui, Alex Mpweku amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kutoa Tshs 400milioni za kujenga kituo cha Afya Shelui.
Pia, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni kwa kukubali kuchangia Tshs 32.1milioni ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati huku ukitumia jumla ya Tshs 400.38milioni chini ya Kikosi kazi cha Corparation Sole Surperitandents.
Mpweku amebainisha kuwa Kikosi Kazi kilianza rasmi kazi Mei 01, 2020 kwa kusafisha eneo ambalo yatajengwa majengo matano na kwa sasa kipo katika hatua ya ufyatuaji wa tofari.
Mpaka mradi unakamilika majengo matano yanatarajiwa kujengwa ambayo ni jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji (theater), nyumba ya mtumishi, jengo la kufulia (laundry), jengo la kuhifadhia maiti(mortuary) na jengo la maabara (laboratory).
Akichangia maoni Diwani wa kata ya Shelui na Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala, Omary Kinota amewakumbusha Wanakamati wa ujenzi huo kuhakikisha wanavaa barakoa ili kuhakikisha wanajilinda na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
Kinota amemtahadharisha Injinia wa Halmashauri hiyo kuwa makini na ardhi ya Shelui.
“Nikuombe Injinia kuhakikisha unafuata maelekezo yanayotakiwa, ardhi ya Shelui sio salama na sio rafiki kwa majengo, hivyo tukilemaa tukaamini kuwa ni sawasawa na sehemu nyingine kwa kweli tutapata hasara,” amefafanua Kinota
MWISHO
Diwani wa kata ya Shelui na Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Omary Kinota (JB) akimtahadharisha Injinia wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Shelui kua makini na ardhi ya Shelui. Picha na Hemedi Munga
Mganga Mkuu wa Zahanati ya Shelui, Alex Mpweku akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa kituo cha Afya Shelui mbele ya Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala. Picha na Hemedi Munga
Wajumbe wa kamati ya ujenzi wa kituo cha Afya Shelui wakisikiliza kwa makini maagizo ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Samwel Shillah alipofanya ziara akiwa na Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala kata ya Shelui kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Shelui. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.