Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Samwel Shillah amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni kuufunga Mwalo uliopo kati ya Mwalo wa Doromoni na Misri mara moja.
Shillah ametoa agizo hilo leo Alhamisi Mei 14, 2020 kando mwa Ziwa Kitangiri Mwalo wa Doromoni alipokuwa katika ziara ya Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala ya Halmashauri hiyo.
Akiongea na baadhi ya Wavuvi na Wenyeji waliopo kando ya Ziwa Kitangiri, Shillah amewaomba Wavuvi hao kulinda rasilimali hiyo muhimu inayoweza kukuza uchumi wao huku akiwataka kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
“Niwaombe tushirikiane kulinda Ziwa hili kwa kuwa ni lakwetu na hatuwezi kufurahia samaki watokao Ziwani ikiwa sisi ni wagonjwa, hivyo lazima tuchukue tahadhari ya covid-19,” amesema Shillah na kuongeza
“ Muhakikishe kila anayefika hapa analipa ushuru kwa sababu ushuru huo ndio unaochangia kuleta maendeleo.”
Halikadhalika, Shillah amewaagiza watendaji wote wa kata Wilayani humo kuhakikisha wanahuisha akaunti za vijiji na kuziwasilisha ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Mapema akiwasilisha maoni yake mjumbe wa Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala ya Halmashauri hiyo, Wilfredi Kizanga Diwani wa Kata ya Tulya. ameikumbusha kamati hiyo kuwa iliahidi kujenga kizimba katika Mwalo wa Doromoni kwa ajili ya kuhifadhi boti na kuwa na wepesi wa kufanya doria.
“Ziwa Kitangiri lina umuhimu mkubwa kwa sababu ni chanzo kizuri cha mapato ya Halmashauri yetu, hivyo ninaiomba kamati hii kuhakikisha inazitatua changamoto zote ili kuongeza tija na mapato,” amesema Kizanga
Akijibu swali la ndugu Juma mmoja wa wenyeji wanaoishi kando ya Ziwa hilo aliyetaka kujua kuwa, wao kama kata au kijiji wananufaika na nini baada ya mapato kupelekwa Halmashauri?
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala ya Halmashauri hiyo, Innocenti Msengi amesema kuwa kamati hua inajadili na kuweka mikakati inayoinufaisha kata ya Kidaru na nyinginezo Wilayani humo kupitia ushuru unaopatikana baada ya kuuza samaki wakubwa kwa wanunuzi watokao maeneo ya ndani na nje ya wilaya.
Naye Afisa Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Deogratius Isagala amesema kuwa Ziwa Kitangiri ni rasilimali muhimu ya Wilaya ya Iramba kwa sabubu limekuwa na mchango mkubwa wa kuboresha lishe na uchumi wa Wananchi.
Amesema kuwa kumekua na changamoto ya ongezeko la uvuvi haramu katika mialo iliyopo Wilaya jirani za Kishapu, Meatu na Igunga.
Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala ya Halmashauri hiyo, imefanya ziara Ziwa Kitangiri lenye ukubwa wa kilometa za mraba 105 na kumalizia ziara hiyo kata ya Shelui kwenye ujenzi wa kituo cha Afya.
Ujenzi huo ulioanza baada ya kupokea fedha Tshs400 milioni kotoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Kupitia fedha hizo majengo matano yanatarajiwa kujengwa ambayo ni jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji (theater), nyumba ya mtumishi, jengo la kufulia (laundry), jengo la kuhifadhia maiti(mortuary) na jengo la maabara (laboratory).
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akiwaagiza wavuvi wote kuhakikisha mgeni yoyote atakayefika Ziwani hapo anasajiliwa ili atambulike anakotoka kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. Picha na Hemedi Munga
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakiwa wameshika samaki watokao Ziwa Kitangiri walipo fanya ziara Mei 14, 2020 Ziwani Hapo. Wakati kati ni Mh, Ester, nyuma yake ni Mh, Innocenti Msengi na Mbele yake ni Mh, Wilfredi Kizanga Picha na Hemedi Munga
Kaimu Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hadhiri Ngayunga alipotembelea Ziwa Kitangiri kukagua ukatishaji wa ushuru utokanao na samaki wa Ziwa hilo. Picha na Hemedi Munga
Mvuvi akiwa na baadhi ya wanunuzi punde baada ya kuwasili toka kuvua katika Ziwa Kitangiri. Picha na Hemedi Munga
Samaki aina ya Pelege waliovuliwa toka Ziwa Kitangiri. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.