Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Wizara ya Maji kupitia kitengo cha maabara yake imetumia takriban Tsh 3.4 milioni kuandaa vitakasa mikono vilivyogawiwa katika shule ya Sekondari Lulumba Wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Vifaa hivyo vimegawiwa leo Julai 04, 2020 katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Lulumba mjini hapa.
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo, Mhandisi Lydia Joseph amewataka wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kutumia vitakasa mikono ambavyo vimetolewa na Wizara hiyo kwa sababu vinaaminika na kuwa na mchanganyiko unaotakiwa.
“Wizara ya Maji ilijihusisha na utengenezaji wa vitakasa mikono vyenye viwango ambavyo vilianza kutumkika katika Wizara hiyo,” amesema Mhandisi Joseph na kuongeza kuwa
“Kwa hiyo katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo akapata wazo la kuisaidia jamii ndogo ya shule ya Msalato Dodoma, shule ya wasichana Tumaini na leo Shule ya Lulumba sekondari Iramba kwa sababu tayari vitakasa mikono hivyo vimewasaidia Wizarani.”
Pia amewataka wanafunzi hao kuendeleza zoezi la usafi kwa kuwa ni kitu ambacho kinafanya afya ya Mwanadamu kuendelea kuimarika.
“Kwa hiyo tabia kama hii ya kutumia vitakasa mikono baada ya kuhisi kuwa umeshika mahali pasipo salama na miundombinu hii ya maji itafanya afya zenu ziendelee kuimarika na kuepukana na magonjwa yakuambukiza na kuweza kufuata masomo vizuri.” ametilia msisitizo Mhandisi
Katika hatua nyingine amempongeza Mhandisi wa Maji RUWASA wa Wilaya hiyo, Ezra Mwacha kwa kuweza kutimiza agizo la Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo alipowaagiza kutengeneza mtambo utakaorahisisha huduma ya kunawa kwa kutumia maji yanayo tiririka ili kuendelea kuchukua tahadhari ya kuepukana na uchafu na magonjwa nyemelezi.
Awali akitoa taarifa fupi ya shule hiyo Mkuu wa Shule, Yeremia Kitiku amesema kuwa shule hiyo inawanafunzi 946 na walimu 30 ambao bado wanaendelea kuchukua tahadhari ya koroka kwa kuwasisitiza wanafunzi kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.
Kitiku amesema kuwa wameendelea kuchukua tahadhari ya kuwapima joto wanafunzi asubuhi na jioni kwa kuzingatia mwongozo na maelekezo yaliotolewa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wataalam wa Afya.
Pia, ameishukuru Serikali kupitia kwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo kwa kushirikiana na SUWASA Singida na RUWASA Iramba kwa kuwaletea mtambo wa kudumu wa kunawaia mikono wanafunzi, walimu na wageni mbalimbali watakaotembelea shule hiyo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Pius Songoma akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Luhahula ameishukuru Wizara ya Maji kwa kuunga juhudi za Mhe, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuhakikisha kwamba watanzania wanakua salama dhidi ya janga la corona.
“Kwa kweli ushupavu na msimamo wa Mhe, Rais John Pombe Magufuli umefanya Watanzania kunusurika na janga la korona, hivyo amemuhakikishia mhandisi huyo kuwa mitambo hiyo itatumika na kutunzwa vizuri.” amesema Songoma
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni amewaasa wanafunzi wa Shule hiyo kuacha tabia yakula mahindi ya Shule.
“Wanangu Wanafunzi wakike msidanganyike na wanaokula mahindi ya shule, kazeni msuli ili mfanikiwe katika maisha yenu, Wanafunzi wa kiume msile mahindi ya shule acheni yakue, yakomae na kuwekwa galani na Walimu wenzangu chungeni mahindi ya Shule.” ameusia Mwageni
Katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi vifaa hivyo vilivyotolewa na Wizara ya Maji pamoja na mamlaka za maji SUWASA Singida na RUWASA Iramba, Wanafunzi mbalimbali wameishukuru Serikali kwa kujali swala la elimu Tanzania.
Akiongea katika hafla hiyo baada ya ugawaji wa vitakasa mikono, Kaka Mkuu wa Shule hiyo, Ernest Munishi ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo utakaowawezesha kuendelea kuchukua tahadhari ya maambukizi ya gonjwa la corona.
Naye Dada Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Paulina Wiliam ameendelea kuishukuru Wizara ya Maji kwa kuwaletea mradi huo wa maji utakowawezesha muda wote kuwa hai na wasafi kwa muda wote wawapo shuleni huku akiwaahidi viongozi hao kuwa watautunza mradi huo kwa ajili ya vizazi vinavyokuja.
MWISHO
Mhandisi Lydia Joseph toka Wizara ya maji akiwafafanulia wanafunzi wa shule ya Sekondari Lulumba kuendelea kutumia vitakasa mikono ambavyo vimetolewa na Wizara hiyo kwa sababu vinaaminika na kuwa na mchanganyiko unaotakiwa. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akipokea kitakasa mikono toka kwa Mhandisi Lydia Joseph toka Wizara ya Maji. Picha na Hemedi Munga
Meneja wa Maji Wilaya ya Iramba RUWASA, Mhandisi Ezra Mwacha akiwaasa wanafunzi kuutunza mtambo wa maji ya kunawia uliotolewa kwa kushirikia na SUWASA Singida. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Shule ya Sekondari Lulumba, Yeremia Kitiku akitoa taarifa fupi ya shule hiyo mbele ya Mwakilishi wa Profesa Kitila Mkumbo, Mhandisi Lydia Joseph toka Wizara ya Maji wakati wa hafla fupi ya kugawa vitakasa mikono vilivyotelewa na Wizara hiyo. Picha na Hemedi Munga
Mhandisi Lydia Joseph toka Wizara ya Maji katikati kushoto ni Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Marietha Kasongo na Kulia ni Afisa Elimu na Taaluma wa Halmashauri hiyo, Patricia Ngaa. Picha na Hemedi Munga
Mhandisi Lydia Joseph toka Wizara ya Maji akiwa na viongozi mbalimbali pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lulumba katika picha ya pamoja baada ya hafla ya ugawaji wa vitakasa mikono vilivyotolewa na Wizara hiyo. Picha na Hemedi Munga
Mtambo wa kunawia uliotolewa na RUWASA Iramba kwa kushirikiana na SUWASA Singida kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Lulumba.Picha Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.