Mhe. Mkuu wa Wilaya Iramba Selemani Y. Mwenda amezindua kifaa cha kisasa cha upimaji ardhi (DGPS S86 RTK) leo tarehe 23/09/2021 katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba chenye uwezo wa kutembea kilometa 30. Akihutubia katika hafla ya uzinduzi huo, amewapongeza kwa pamoja Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Innocent Msengi na Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Michael Matomora kwa kufanikisha kununua mitambo ya kisasa ya upimaji ardhi aina ya DGPS S86 inayotumia teknolojia ya Real Time kinematics (RTK).
“Nawapongeza kwa namna ya pekee sana, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkururgenzi Mtendaji wetu kwa tukio hili la kununua kifaa hiki cha Upimaji, kwa maana sisi Wanairamba tumekuwa Wilaya ya kwanza katika Mikoa hii ya Kanda ya Kati kununua kifaa hiki, hiki kifaa tunakihitaji sana kwa sasa, hakika tumetimiza malengo na maagizo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Hatua hii ya kununua na kumiliki kifaa hiki kitatuwezesha kutekeleza zoezi hili la utambuzi wa ardhi, kupanga, kupima na kurasimisha Matumizi Bora ya Ardhi katika Wilaya yetu” alisema Mhe. Mwenda
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Shelui, Mhe. Mwenda alisema “Mmeelezwa faida za kifaa hiki, mtakumbuka kwamba, nilipokuwa nafanya ziara katika kata hii, mlisema kero zenu za migogoro ya ardhi ikiwemo mipaka ya vijiji, vitongoji na tatizo kubwa la viwanja kukosa mpangilio mzuri, wengine wanajenga barabarani, Niwahakikishieni kuwa uzinduzi wa kifaa hiki cha upimaji tutawapimia ardhi zenu na kuwapatia hati zenu kwa kutumia mitambo hii mipya ya kisasa; amesisitiza Mhe. Mwenda
Akiongea na wananchi, Katibu wa chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iramba Ibrahimu Mjanaheri alisema “Nawapongeza sana Halmashauri kwa kununua mtambo huu wa upimaji. Sisi lazima tuwaelekeze njia iliyonyooka wananchi ili msikae vijiweni na kudanganyana. Sheria ya ardhi inasema ardhi yote ni mali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Bila kuwa na hati ya ardhi huwezi kumiliki ardhi na ikitokea serikali inataka kuweka mradi kwenye ardhi yako na huna hati ya ardhi huwezi kupata fidia, Nawashauri changamkieni hii fursa ya kupimiwa, kurasimishiwa makazi na kupata hati miliki ya ardhi yako.
Tunamshukuru sana Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea Mkurugenzi mwenye akili nyingi, Mpaka sasa tayari tumechagua Kata saba kati ya 20 za kuanzia kupima ardhi ikiwa ni Pamoja na ulemo, oldkiomboi, kiomboi, shelui, ndago, kinampanda na kyengege, hivyo nataka uongozi wa Chama ushiriki kuhamasisha wananchi kupimiwa maeneo yao na kila mwezi tupeane taarifa za utekelezaji; alisisitiza Mjanaheri.
Aliongeza Kusema “NMB wamesema kwa lugha rahisi sana, nenda NMB ukakope fedha kwa ajili ya kurasimishiwa ardhi yenu. Natamani kesho nisikie wananchi wa kata ya Shelui wanahitaji kurasimishiwa maeneo yao. Kuweni wa kwanza kuchangamkia fursa hizi.
Niwaombe sana, kifaa hiki kisiende kufanya kazi sehemu nyingine, kimalize kwanza hapa ndio wengine wakiazime. Miji yote iliyo kando ya barabara kuu hii ya lami itokayo Dodoma kwenda Mwanza yaani Maluga, Shelui, Kyengege, Ulemo, Misigiri ina sifa ya kuwa mji mdogo lakini lazima ipimwe ndipo itambuliwe kama Miji midogo; alisisitiza Mjanaheri
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mhe. Innocent Msengi amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na ushirikiano wa pamoja katika kuleta maendeleo katika Wilaya ya Iramba “Najua wengine mmetoka sehemu mbalimbali, mmefanya jambo jema, kikubwa zaidi twende tukaifanye kazi halisi ya upimaji kupitia kifaa hiki tulichokinunua kwa fedha zetu wenyewe, niwashukuru sana Baraza la Madiwani kwa Mshikamano huu na kufanikiwa katika jambo hili la kununua kifaa hiki cha kisasa cha upiamaji ambacho kitaleta uchumi kwenye Wilaya yetu kupitia sekta ya ardhi. Hivyo Naomba tushikamane tulete maendeleo zaidi kwenye Halmashauri yetu.
Tukasimamie miradi ya maendeleo na mapato kwa pamoja. Leo tumenunua kifaa hiki, lakini yapo mambo mengine ambayo tunatakiwa tuyatekeleze kwa pamoja, Alisisitiza Mhe. Msengi .
Akiongea na wananchi wa Kata ya Shelui, Mtaa wa Nselembwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mhandisi Michael Matomora amesema “Kifaa hiki kimenunulia kwa fedha za wananchi wenyewe, hivyo basi suala la kupima ardhi ni sera ya Chama cha Mapinduzi na utekelezaji wake ni kwa nchi nzima na kwamba ni takwa kisheria, kila kipande cha ardhi cha nchi hii kitapaswa kitambuliwe, kipangwe na kipimwe, kwahiyo hakuna mjadala tena kwenye suala la kupima na kurasimisha makazi, jambo ambalo linasimamiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mama Samia suluhu Hassan,
Aliongeza kusema “Moja ya jukumu aliloniagiza wakati ananiteua ni kuhakikisha ardhi ya Wilaya ya Iramba inapimwa. Tumenunua kifaa hiki kwa ajili ya kutekeleza agizo hilo na tutahakikisha tunawapimia ardhi yenu na kuwapatia hati za kumilikishwa ardhi kisheria”. Alisisitiza Mhandisi Matomora
Kama mlivyosikia hotuba ambayo imesomwa sasa hivi na afisa ardhi wa Wilaya, leo ni rasmi sasa kwa Iramba tunazindua zoezi la kuthaminisha na kutoa hatimiliki za ardhi kupitia fursa ya Mikopo itakayotolewa na Benki ya NMB. Niwafahamishe tu kwamba Benki ya NMB imeungana na Serikali yetu pendwa ya awamu ya sita, kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwawezesha wananchi kupata hatimiliki ya ardhi zao. Fursa hii, Benki ya NMB inaenda kutoa mikopo kwa wamiliki wote wa ardhi ambao hawana hati, pale inapopimwa Benki iko tayari kutoa mkopo kukuwezesha kwenye mambo matatu:
Jambo la kwanza; Kuthaminisha ardhi (survey and planning). Jambo la pili ni; usajili wa Hati -Benki inaenda kutoa mikopo kuanzia elfu hamsini mpaka milioni moja. Na hii gharama yote itatolewa na wizara ya ardhi kupitia Benki ya NMB nchini kote Tanzania. Kwa watu wote ambao Wizara itawarasimishia makazi basi ni kwamba wizara ya ardhi itatuletea sisi majina ya wananchi waliorasimishiwa makazi yao na thamani ya mkopo ambao mtu atapewa. Kwa hiyo watu wote ambao watapitiwa na zoezi hili wanafursa kubwa ya kuja NMB kuchukua mkopo wa kufanya upimaji na usajili wa hati zao.
Akisoma taarifa ya uzinduzi wa mpango wa urasimishaji makzi, ndg Velarian Msigala amesema “Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilizindua rasmi Mpango mpya wa Urasimishaji Makazi mnamo tarehe 11/08/2021 Wilaya ya Mbalali Mkoani Mbeya.
Leo, tarehe 23/09/2021 tunauzindua rasmi kwenye Wilaya yetu ya Iramba hapa Mtaa wa Nselembwe. Na mikutano ya uhamasishaji itaendelea kwenye Kata zingine.
Mpango huu ni wa fursa ya kila Mwananchi kukopeshwa fedha na Benki ya NMB kwa ajili ya kufanya Utambuzi wa Miliki ya ardhi, Upangaji, Upimaji na Umilikishwaji kwa kupata Hati Miliki.
Lengo kuu la mpango ni kuhakikisha kila mwananchi anayeishi Mjini na maeneo ya Vijijini yenye Mpango wa Matumizi Bora ya ardhi anamilikishwa ardhi yake kwa kupata Hati Miliki.
FAIDA ZA KURASIMISHA ARDHI NA MAKAZI
. Kuishi kwenye makazi bora yaliyopangwa na kuwekewa miundombinu muhimu
mfano barabara, umeme, maji, mifereji ya maji taka n.k
. Kuongeza thamani ya ardhi, unapomiliki ardhi iliyopangwa na kupimwa thamani
yake inapanda juu kwa kuwa umiliki wako unatambulika kisheria.
. Kupunguza na kuondoa migogoro ya ardhi hasa ya mipaka kati ya majirani.
. Ardhi iliyopangwa na kupimwa ina fursa kubwa kukuinua mwananchi kiuchumi hasa
Hati miliki inapotumika kama dhamana katika taasisi za kifedha katika kutafta mikopo
URASIMISHAJI MAKAZI
Halmashauri ya Wilaya Iramba kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iligawa Mitaa Miwili tu ya Misigiri na Shelui kwa Kampuni ya Mosaic Company (T) ltd, kwa ajili ya kurasimisha makazi kwa lengo la kupanga na kupima Viwanja 10,000. Idadi ya Viwanja vilivyotambuliwa Mtaa wa misigiri ni 1,769 na viwanja 108 upimaji wake umekamilika tayari wananchi kumilikishwa. Na kwa Mtaa wa Nselembwe Idadi ya Viwanja vilivyotambuliwa ni 2578 na viwanja 1102 upimaji wake umekamilika, hatua ya ukamilishaji kikokotoo cha gharama za umilikishwaji kwa viwanja hivyo zinaendelea katika Ofisi ya Kamishna wa ardhi Mkoa.
MPANGO MKAKATI WA WILAYA
Kufutia ununuzi wa Mitambo ya Kisasa ya Upimaji ni kwamba Halmashauri ya Iramba
Fursa hii pekee, tutaisimamia kikamilifu ili kuhakikisha Halmashauri ya Iramba inakua kiuchumi kupitia Sekta ya ardhi katika Mpango wa Urasimishaji makazi unaozinduliwa rasmi leo tarehe 23/09/2021.
MWISHO.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.