Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amepokea vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Tsh 9.1milioni vya kujikinga na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba na Wadau Wengine.
Luhahula amepokea vifaa hivyo leo Alhamisi Mei 14, 2020 katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Halmashauri hiyo mjini hapa.
Akiongea katika hafla hiyo Mkuu huyo wa Wilaya, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni pamoja na Madiwani wote kwa kununua vifaa vya kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya homa kali inayosababishwa na virusi vya korona.
Amesema Halmashauri hiyo imetoa Tsh 5milioni huku wadau mbalimbali wakijitolea zaidi ya Tsh 4.1milioni.
“Nimshukuru Mkurugenzi Mtendaji Linno Mwageni na wadau ambao tulikutana nao Aprili 28 mwaka huu kujadiliana kuhusu timu ya Karantini ya vijana 35 ambayo inasaidia kutoa elimu pamoja na kushughulikia uchukuaji wa tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona katika Wilaya yetu ili kuwakinga wananchi wetu” amesisitiza Luhahula na kuongeza
“Tunashukuru kuambiwa na Mkurugenzi Mtendaji kuwa tayari wameshanunua ndoo 63 za kunawia za kukanyaga, sabuni pamoja na mavazi rasmi pea 40 za PPE (Personal Protective Equipments) ya kujikinga wakati wakutoa huduma.”
Katika kuendelea kupambana na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba amechangia ndoo 48.
Luhahula amefafanua kua ndoo hizo zilizotolewa na Dkt. Mwigulu Nchemba zimepelekwa katika kila ofisi ya Mtendaji wa kata na ofisi ya kata ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo.
Halikadhlika, Luhahula amesema kua wameweka utaratibu wa kupima joto watu wanaokuja kwenye msiba kutoka nje ya wilaya hiyo, hivyo endapo atapatikana mmoja wapo ana dalili za ugonjwa huo, nyumba hiyo yenye msiba itawekwa karantini kwa siku 14.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni amesema kua Halmashauri imetekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kuhusu kila Halmashauri kununua vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa corona pamoja na kununua vifaa vya kunawia kwa Zahanati 29, vituo vya Afya 4 na Hospitali ya Wilaya.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Samwel Shillah amesema kuwa tayari wananchi wamekwisha elewa utaratibu wa kupima joto kuwa ni wakawaida.
Utaratibu huo umesaidia mtu kujua hali yake na kuwa eneo analokwenda ni salama kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akinawa maji yanayotiririka kutoka katika ndoo mojawapo kati ya zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akimkabidhi Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Timothy Sumbe PPE na Sabuni. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni kwa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona alivyomkabidhi. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akifafanua namna alivyotekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.