Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Linno Mwageni amewataka Wenyeviti wa bodi za maji, Wawakilishi wa Wanawake katika bodi za maji, Wahasibu wa jumuiya na Makatibu wa Jumuiya kutoa huduma bora ya maji katika maeneo yao ili jamii iweze kunufaika na huduma hiyo.
Mwageni ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokua akiongea na wajumbe hao katika kikao kazi cha Mkutano Mkuu wa Nusu Mwaka wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) uliofanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mjini hapa.
“Niwaombe wajumbe kutoa huduma za maji zilizokua bora zitakazo mnufaisha mwananchi kwa sababu yeye ndio mlengwa aliyesogezewa huduma za maji vijijini,” amesema Mwageni na kuongeza kuwa
“Mnajukumu kubwa la kuhakikisha mnasimamia kanuni na taratibu za uanzishaji na uendelezaji wa jumuiya za maji vijijini kwa lengo lakutoa haduma bora na sio kuathiri jumuiya hizo.”
Amewataka Wenyeviti wa vijiji na Watendaji wa kata kusimamia Jumuiya za maji ili kuziba mianya ya kuvujisha fedha na kuwa kila fedha itakayopatikana ipelekwe benki.
“Mkilitekeleza hilo mtasaidia fedha zinazopatikana kuendelea kupanua mradi wa jumuiya na kuweza kuwafikia wananchi mahala ambapo mradi ulikua haujafika,” ametilia mkazo Mwageni
Kwa upande wake Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovison Ntangeki ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Luhahula katika hotuba yake amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuwekeza ujenzi wa miradi ya maji vijijini kwa kuwashirikisha wananchi kuibua, kupanga, kutekeleza, kusimamia na kuendesha miradi hiyo pindi itapokamilika.
“Ndugu zangu Wajumbe fahamuni kuwa ni kosa kisheria kwa chombo chochote kinachotaka kutoa huduma ya maji vijijini pasipo kusajiliwa kwa mujibu wa sheria namba 5 ya 2019 inayomtaka mwendeshaji kupata leseni ya kutekeleza jukumu hilo, hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au chombo hicho,” amesema Ntangeki kwa niaba ya Mkuu huyo
Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa sheria mpya ya uundaji wa jumuiya za maji vijijini, Meneja wa Maji wa Wilaya hiyo,Mhandisi Ezra Macha amesema jumuiya 14 zimeisha kamilisha taratibu za uhuishaji huku vijiji vitatu vya Meli, Nselembwe na Nguvumali vikiwa katika hatua za ukamilishaji wa taratibu za usajili.
Macha amewaambia wajumbe hao kuwa fedha za jumuiya zitabaki kuwa za jumuiya kwa kufuata sheria hii ambayo imeingiza wataalam katika bodi ya maji ili kuongeza uwajibikaji na utaalam katika kusimamia jumuiya za maji ngazi ya jamii ili ziwe endelevu zenye ufanisi na upatikanaji wa fedha.
Naye mmoja wa washiriki wa Mkutano huo toka kata ya Mukulu Wilayani hapo, Eliya Sauti amewaomba viongozi wa RUWASA kufika vijijini mara kwa mara kwa lengo la kuendelea kutoa elimu ya mabadiliko ya sheria hiyo.
MWISHO
Meneja wa Maji Wilayani Iramba, Mhandisi Ezra Macha akizihakikishia jumuiya za maji kuwa fedha za jumuiya zitabaki kuwa za jumuiya kwa kufuata sheria Na 5 ya mwaka 2019 ambayo imeingiza wataalam katika bodi ya maji ili kuongeza uwajibikaji na utaalam katika kusimamia jumuiya za maji ngazi ya jamii ili ziwe endelevu zenye ufanisi na upatikanaji wa fedha. Picha na Hemedi Munga
Afisa Tawala wa Wilaya ya Iramba, Dijovison Ntangeki akigawa vyeti kwa jumuiya za maji vijijini zilizokwisha kamilisha usaji kwa mujibu wa Sheria Na, 5 ya mwaka 2019. Picha na Hemedi Munga
Wenyeviti wa bodi za maji, Wawakilishi wa Wanawake katika bodi za maji, Wahasibu wa jumuiya na Makatibu wa Jumuiya wakifuatilia maelekezo mbalimbali toka kwa wataalam namna ya kuziendesha jumuiya zao kifanisi. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.