Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida – Iramba. Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi alizozitoa kwa ajili ya kufungua barabara za vijijini na mijini mkoani humo.
Dkt. Mahenge ametoa pongezi hizo leo Alhamisi Januari 27, 2022 wakati alipofanya ziara ya kukagua barabara mbalimbali zinazotengenezwa wilayani Iramba.
“Tunakila sababu za kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa fedha za tozo kwa sababu zimeleta mafanikio makubwa.”
Aidha, aliongeza kuwa haijawahi tokea kupata fedha nyingi namna hii katika levo ya mkoa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini ukilinganisha na zamani ambapo TANRODI walikuwa wakipewa fedha chache.
Halikadhalika, Dkt Mahenge amewataka TARURA kutafuta fedha za kujenga daraja katika mto Kinshoka ili barabara hiyo ziweze kupitika wakati wa masika na kiangazi.
“Niwaombe TARURA muhakikishe katika mipango yenu yote mnazingatia ujenzi wa daraja katika mto kinshoka kwa sababu ndio mtaweza kuwasaidia hawa wananchi na kuifanya miundombinu hii kuwa na thamani.” Alisema
Pia amempongeza Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi na Waziri wa fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuanziasha na kusimamia fedha za tozo ambazo leo zimewezesha upatikanaji wa barabara hii.
Akielezea hali halisi ya jumla ya fedha ambazo mkoa wa Singida umezipata toka katika vyanzo mbalimbali Meneja wa TARURA mkoa wa Singia, Mhandisi Tembo David alisema kuwa mkoa umepata zaidi ya Tsh bilioni 20 ambapo Tsh 4 bilioni ni za mfuko wa jimbo na kila jimbo limepata Tsh 500 milioni.
Tembo amemuhakikishia Mkuu wa mkoa huyo kuwa wakandarasi wote waliopata kazi za kutengeneza barabara watakamilisha kwa wakati kwa sababu ratiba zao zinaruhusu kufanya kazi hata katika kipindi hichi ambacho imedaiwa kuwa mvua ni chache.
Aidha, aliongeza kuwa wanatarajia kuwa miradi hii ikikamilika itafungua shughuli za uchumi kwa wananchi wa Iramba na Singida kwa ujumla.
Awali akisoma taarifa fupi mbele ya mkuu wa mkoa huo meneja wa TARURA Iramba, Mhandisi Evance Kibona alisema kuwa wanafedha takribani Tsh 454.5 milioni ambazo zinatengeneza barabara ya Shelui Nkyala yenye urefu wa kilometa 5, fedha Tsh 524.4 milioni ambazo ninatengeneza barabara ya Shelui Tintigulu yenye urefu wa kilometa 7.3, fedha Tsh 219.8 milioni kwa ajili ujenzi wa barabara ya Urughu Mlandala yenye urefu wa kilometa 10 pamoja na fedha Tsh 545.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Urughu, Mahola na Mpujizi yenye urefu wa kilometa 9.
Barabara hizi zinatengenezwa kutokana na fedha ambazo zinatoka serikali kuuu, fedha za mfuko wa jimbo na fedha ambazo zinatokana na tozo.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.