Na hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida – Iramba. Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge amewahamasisha wananchi wote kulima zao la alizeti pamoja na mazao mengine kwa kadri wanavyoweza.
Dkt Mahenge ametoa wito huo leo Alhamisi Januari 27, 2022 alipofanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara katika kata ya Urughu wilayani Iramba.
“Ndugu zangu huu ni msimu wa kilimo kila mmoja afanye kazi kwa sababu barabara zinajengwa ili msafirishe mazao yenu.” Alihamasisha Dkt Mahenge
Aidha, aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza serikali ya Mheshimiwa Rais Samia imeweka ruzuku katika mbegu ya alizeti ambapo ukienda dukani na kuambiwa mfuko wa mbegu ya alizeti unauzwa mfano wa Tsh 7000 basi mwananchi atachangi Tsh 3500 na serikali kumuongezea Tsh 3500.
“Haijawahi kutokea mkoa wa Singida tumepewa tani 465 zenye thamani ya takribani Tsh 3 bilioni, hivyo niwashawishi ndugu zangu twendeni tukalime.” Alihamasisha Mkuu wa Mkoa
Pia aliwaeleza kuwa katika kampeni ya mkoa kulima zao la alizeti bado haijafunga milango kwa mkulima mabaye anahitaji kulima zao la mtama, mahindi, pamba na mazao mengineyo kulingana na uwezo wao na utashi.
Halikadhalika, Dkt Mahenge alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuwapeleka watoto ambao wamefaulu shule kwa sababu elimu ndio urithi wao utakao wakomboa katika maisha haya.
“Ndugu zangu niwaombe mpeleke watoto shuleni kwa sababu shule zimeishafunguliwa zikiwa na madarasa yakutosha, madawati yakutosha na walimu wakutosha.”
Alifafanua kuwa elimu ndio ufunguo utakaomkomboa mwanafunzi na kuweza kujiajiri na pindi atakapopewa fedha anaweza kufanya biashara kwa ufanisi.
Awali akielezea hali ya barabara katika kata ya Urughu wilayani Iramba Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda alionesha furaha yake kwa wananchi hao baada ya kuona kuwa kero walizowasilisha kwake kipindi alipofika kusikiza kero zimetatuliwa.
“Ndugu zangu ni baada ya miezi minne tangu muwasilishe kero ya barabara kwangu na serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imewatimizia ujenzi wa barabara na leo Mkuu wa mkoa amekuja kuzikagua.” Alisema Mwenda
Kwa upande wake diwani wa kata ya Urughu wilayani hapo, Simon Tyosela akamuomba Mkuu huyo wa mkoa kuwafikishia salamu zao za pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwatatulia kero ya barabara.
“Mkuu wa mkoa tunashukuru sana kwa kufika kwako hapa tunaomba utufikishie salamu kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa sababu hajawahi kufika huku lakini ametujali sana maana wilaya ya Iramba inakata 20 lakini katika kata yetu ametupatia takribani Tsh 1.5 bilioni ukilinganisha na kata nyingine.” Alisema Tyosela
Naye mmoja wa wananchi wa kijiji cha Urughu wilayani hapo, Mohammed Salehe alimshukuru mkuu huyo wa mkoa kwa kuwatembelea na kumuomba afike hapo mara kwa mara.
Salehe alisema kuwa serikali hii ni nzuri kwa sababu inaleta maendeleo katika kata yao.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.