Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amefanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa takribani Tsh 2.4bilioni ikiwa ni ahadi ya Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Dkt Nchimbi amefanya ziara hiyo leo Al hamisi juni 18, 2020 Tarafa ya Ndago, Shelui na Kisiriri Wilayani humo.
Akiongea na wananchi katika sehemu tofauti tofauti Mkuu huyo wa Mkoa amesema ziara yake pamoja na kukagua miradi ya maendeleo pia kuona namna ambavyo wananchi wanamuona Mhe, Magufuli katika maisha yao kupitia miradi ambayo ameitekeleza.
“Mimi ninataka nijue wananchi hawa wakiangalia jengo hili wanamuona Mhe,Magufuli? Wanafunzi hawa wakiwa hapa wanamuona Mhe, Magufuli?” ameuliza Dkt Nchimbi nakuongeza kuwa
“Mhe, Magufuli ambaye ameongeza thamani ya maisha na akaleta mabadiliko ya maisha kwa wananchi wa Iramba, hivyo wananchi hawa wakatambua kuwa hakika aliyetufanyia haya ni Mhe, Magufuli na lazima nimpe kura yangu.”
Kutokana na wananchi mbalimbali kumueleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa wanamuona Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli katika maisha yao kwa namna alivyowaletea maendeleo ya shule za kidato cha tano, nyumba za walimu, mabweni, mabwalo, maji, umeme na barabara za lami.
“kwa kuona bweni, nyumba na majengo haya tunamuona Mhe, Rais Magufuli ambaye ametuletea amani katika mioyo yetu kwa sababu wanafunzi watakua kwenye mahali penye staha na wazazi wakiwa na amani kwa kuwa watoto wao wapo katika maeneo salama, mazuri na kupata uelewa wa masomo,” amesema Dkt Nchimbi
Halikadhalika wananchi watakua na utulivu na kuweza kupanga shughuli zao za kiuchumi kwa kuwa ni kizazi bora kinacholelewa na Mhe, Rais John Magufuli.
“Tumewasikia hapa mama lishe, bodaboda na wengine kuwa wanatunzwa na Mhe, Rais John Magufuli, na hivyo kuona mabadaliko ya thamani katika maisha yao ambayo yameletwa na mambo makubwa na mazuri ambayo yamefanywa na Mhe, Rais John Magufuli.” ameongeza Mkuu wa Mkoa na kufafanua kuwa
“Na sisi tupo tayari kumrudisha kitini tena kwa kua yeye ametuhakikishia amani,afya, upendo, uzima, utulivu, mshikamano, maendeleo na uhakika wa maisha yetu kuwa tutatoka hapa na kufika mbele.”
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni kujiandaa na ujenzi wa eneo la kupumzikia wakati watu watakapokua wakiwasubiria wazazi katika kituo cha Afya Shelui kinachojengwa kwa fedha zilizoletwa na Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli punde ujenzi utakapokua umekamilika.
Katika ziara hiyo wataalamu mbalimbali wametoa ufafanuzi wa namna miradi inayvotekelezwa katika maeneo yao ilivyogusa jamii katika Nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu.
Akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa miundombinu ya nyumba, bweni na bwalo vinavyojengwa Shule ya Sekondari Ndago kwa ajili ya kidato cha tano, Mkuu wa Shule hiyo, Genatio Fungo amesema walipokea takribani Tsh 225milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba (2in1), bweni na bwalo.
Fungo amesema Wanafunzi, Walimu wa shule ya Sekondari Ndago na Jamii kwa ujumla watanufaika kwa uwepo wa makazi ya Walimu, kutoa malazi kwa Wanafunzi wa kidato cha tano na bwalo la chakula litakalotumika kwa ajili ya kulia chakula, kuendeshea mikutano na mitihani mbalimbali.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Hussein Sepoko ameishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe, Rais John Magufuli kwa kuleta Tshs 400milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kijiji cha Nselembwe kata ya Shelui Wilayani hapa.
Sepoko amefafanua kuwa mradi huu utakapokua umekamilika utaweza kuhudumia takribani wananchi 13,550 wa vijiji 5 na vitongoji 23 vya Tarafa ya Shelui.
Naye Mkandarasi anaye jenga barabara ya mchepuo kwenda Hospitali kongwe ya Old Kiomboi amesema takribani Tsh 1.5bilioni zimetumika kukamilisha ahadi ya Mhe, Rais John Magufuli wakati wa kampeni 2015.
Mhandisi amesema kuwa barabara hiyo ina makaravati 15, vivuko 20 vya watembea kwa miguu vyenye upana wa mita mbili huku akimuahidi Mkuu huyo wa Mkoa kuwa wanamalizia uwekaji wa alama za barabarani pamoja na upakaji wa rangi.
Naye Mkuu wa shule ya New Kiomboi, Amadeus Kiduu amesema kuwa gharama ya ujenzi wa bweni la wasichana New Kiomboi utagharimu takribani Tsh 189.2milioni na kuweza kuwanufaisha wanafunzi wa kike kwa kupata malazi, hivyo kuboresha mazingira ya kujifunzia, kupunguza idadi ya wanafunzi wanaotembea umbali mrefu, kuondoa mimba za utotoni na kuongeza muda wa kujisomea kwa pamoja ambapo itachangia kuinua kiwango cha taaluma na ufaulu mzuri.
Akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake kaka mkuu wa Shule ya Sekondari Ndago, Stivin Emmanuel amemshukuru Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jonh Magufuli kwa kutoa ridhaa ya wanafunzi kurudi shule juni 29 mwaka huu.
Pia, amemshukuru Rais kwa ajili ya fedha alizozitoa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu, bweni na bwalo kwani ilikua ni usumbufu walipokua wanapata chakula wakiwa nje, hivyo kwa miundo mbinu hii itawawezesha kuinua taaluma zao na kuweza kufaulu vizuri.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akikagua ujenzi wa kituo cha Afya Shelui kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula na anayemfuatia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni na kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Hussein Sepoko. Picha na Hemedi Munga
Mradi wa bweni la wanafunzi kidato cha tano linalojengwa shule ya sekondari Ndago. Picha na Hemedi Munga
Mradi wa bwalo linalojengwa Shule ya Sekondari Ndago kwa ajili ya wanafunzi wa kitado cha kwanza hadi cha tano. Picha na Hemedi Munga
Mradi wa majengo mbalimbali ya ujenzi wa kituo cha Afya Shelui uliotembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akikagua mradi wa barabara inayokwenda Hospitali ya Old kiomboi Wilayani Iramba ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alipoahidi wakati wa kampeni mwaka 2015. Picha na Hemedi Munga
Mradi wa bweni la wanafunzi wa kike kidato cha kwanza hadi cha nne Shule ya New Kiomboi Mjini Kiomboi Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.