Hemedi Munga, Irambadc
Iramba, Mkuu wa Mkoa wa Singida DKt, Rehema Nchimbi amewaagiza Makamanda wa TAKUKURU waliopo katika Wilaya zote za Mkoa wa Singida kuwafuatilia Wanasheria na Mahakimu umiza ambao huweka Mahakama zao na kuwafundisha wananchi mambo yasiokua sahihi kwenye mwenendo wa kesi husika.
Dkt, Nchimbi ametoa agizo hilo leo Januari 23, 2021 wakati akiongea na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya kuongoza kuingia katika wiki ya sheria Nchini katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri Mjini Kiomboi.
‘’ Ndugu viongozi wenzangu, ningependa viongozi wengine waje kujifunza kwa Makamanda wa TAKUKURU waliopo Iramba na Mkalama namna mtakavyotokomeza tatizo la Mahakimu wanaokiuka sheria kwa kuwaumiza wananchi wenye mashauri mbalimbali katika mahakama zetu,’’ ameagiza Mkuu wa Mkoa na kuongeza kuwa
‘’ Tunawajibu wa kuipenda sheria, kuifahamu sheria na kuiishi sheria ili kutokufanya makosa na kufahamu kuwa hakuna mtu aliyekua juu ya sheria, hivyo tuwe na tabia ya kutii sheria bila shuruti.’’
Halikadhalika amewataka Mahakimu kuwa na tabia za kutoa elimu ya sheria na utendaji kazi wake kwa jamii kwa sababu itaifanya jamii kutofanya makosa na kuwa watiifu wa sheria bila shuruti.
Katika hatua nyingine Dkt, Nchimbi amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Viongozi wa Dini kulinda barabara zilizopo katika Wilaya zao.
‘’ Ndugu washiriki ! tunafahamu kuwa kwa Mungu hakuna kona ya ajali, hivyo Mahakimu hawa wanatumia barabara hizi ni lazima wawe salama,’’ ametilia mkazo Mkuu wa Mkoa
Katika kuchambua maana ya sheria, Mkuu wa Mkoa, Dkt, Nchimbi amewataka Viongozi hao kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka kuwa sheria ipo ndani ya mfumo wa Mwanadamu kwa kuwa kila kiungo cha Mwanadamu kimekaa kwa kutii sheria.
Awali akitoa maelezo ya utangulizi wakati wa kuingia katika wiki ya sheria Nchini, Hakimu Mkazi Mfawidhi anayeshughulikia Wilaya ya Iramba na Mkalama , Christopher Makwaya amesema kuwa lengo la kukutana katika hafla hii ni kutoa elimu ya shughuli za Mahakama katika utendaji wa haki.
Akisoma kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka 2021 isemayo ‘’ Miaka 100 ya Mahakama Kuu, Mchango wa Mahakama katika kujenga Nchi inayozingatia uhuru, haki, udugu, amani na ustawi wa wananchi 1921 – 2021’’ Hakimu Makwaya amesema kuwa Mahakama ya Wilaya ya Iramba imedhamiria kufanya tathimini na kupokea maoni toka kwa wadau kuhusu utoaji wa huduma ya kimahakama.
‘’ Ndungu zangu niombe tufahamu kuwa sisi viongozi wa umma tunawajibu wa kufanya yaliokua mema kwa sababu jamii inatarajia huduma bora kutoka kwetu’’ amesisitiza Makwaya
Katika kuhakikisha Mahakama inatoa huduma bora kwa jamii, Makama imeboresa utoaji huduma za nakala za hukumu na mienendo ya mashauri iitwayo Posta Mlangoni na huduma ya ufunguaji wa kesi kwa njia ya mtandao iitwayo (electronic filing).
Pia amesema kuwa Mahakama Wilayani humo imefanikiwa kupunguza mashauri kwa kiwango kikubwa kati ya mashauri yaliopokelewa mwaka 2019/ 2020 ni 454 nakufanikiwa kuyasikiliza mashauri 361 na kubakiwa na mashauri 83.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa hafla hiyo fupi, Afisa Tarafa wa kata ya Shelui, Nicholaus Makoye amesema kuwa mimba za wanafunzi zitakoma kwa kuitaka jamii kutii sheria bila shuruti kwa kushirikiana kutoa elimu na kupambana na watu wasiowatakia mema wanafunzi kwa kuwasababisha kupata mimba.
Katika kuingia katika wiki ya sheria Nchini zimewasilishwa mada ya ndoa na talaka, mirathi, dhamana, walinzi wa amani, maadili, kesi za jinai na elimu ya uhamiaji.
Uzinduzi wa wiki ya sheria utazinduliwa rasmi Januari 24 na Mhe, Makamu wa Rais, Samia Suluhu na kilele chake kuhitimishwa Februari 1, 2021 na Mhe, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Mwisho
Hakimu Mkazi Mfawidhi anayeshughulikia Wilaya ya Iramba na Mkalama, Christopher Makwaya akielezea lengo la kukutana katika hafla ya kuingia katika wiki ya sheria Nchini kuwa ni kutoa elimu ya shughuli za Mahakama katika utendaji wa haki. Picha na Hemedi Munga
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Wilayani Iramba, Mhe. Rehema Uroki akiwaelezea viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya kuingia katika wiki ya sheria Nchini mada ya mirathi na umuhimu wa kutoa usia namna unavyosaidia ugawaji wa mirathi. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Mkoa Dkt, Reheme Nchimbi akiwa na Viongozi mbalimbali pamoja na Waheshimiwa Mahakimu katika picha ya pamoja punde baada ya kuongoza kuingia katika wiki ya sheria Nchini. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.